DC MEATU AWAAGA WATOTO 36 KWENDA KUFANYIWA UPASUAJI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com



Mwandishi wetu
Meatu, Simiyu – Mkuu wa wilaya ya Meatu, mkoa wa Simiyu, Fauzia Ngatumbura amewaaga Watoto 36 kutoka vijiji 16 vinavyozunguka Pori la Akiba la Maswa,kwenda kufanyiwa kufanyiwa upasuaji wa miguu vifundo (clubfoot), matege (bow legs/knockknees) na midomo sungura (cleft lip and palate) kwa ufadhili ta kampuni ya Utalii ya Mwiba Holdings Ltd.
Kampuni ya Mwiba ambayo ni kampuni tanzu ya Fredkin Conservation Fund(FCF) Imewekeza shughuli za Utalii,wilayani Meatu.mkoa wa Simiyu na imewasafirisha watoto hao, kutoka Meatu hadi mkoani Arusha, katika kituo cha Kafika house ambacho kimekuwa kikitoa huduma ya matibabu hayo.
Akizungumza wakati wa kuagwa watoto hao, Mkuu wa wilaya ya Meatu, Ngatumbura alishukuru kampuni hiyo ya Mwiba kugharamia matibabu ya watoto hao na kuwataka wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto walemavu ama kuhusisha ulemavu na mambo ya kishirikina.
"Leo watoto 36 wanakwenda kupatiwa matibabu katika awamu ya kwanza kati ya watoto 53 wenye uhitaji na mwaka jana watoto 28 walifanyiwa upasuaji na sasa wamepona kabisa, tunapongeza wawekezaji hawa kwa msaada huu na tunaimani wataendelea kusaidia jamii"alisema
Mkuu huyo wilaya alisema msaada huo una manufaa makubwa kwani wazazi wasingeweza kugharamia matibabu ya watoto hao kutokana na kugharimu fedha nyingi.
"Sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na mwekezaji huyo kusaidia jamii na tumepokea maombi ya wananchi huduma hii kutolewa wilaya nzima badala ya vijiji 16 pekee tutamuomba mwekezaji kupanua huduma ili watoto wengi zaidi wapate huduma hii"alisema
Meneja miradi wa Mwiba Holdings, Sylvester Bwasama akizungumza na waandushi wa habari alisema mwaka jana walipatikana watoto 63 ambao walikuwa na uhitaji wa upasuaji lakini waliofanyiwa watoto 28 na mwaka huu, waliongeza uhamasishaji watu kujitokeza ambapo mwaka huu,watoto 131 walipatikana na 53 watafanyiwa upasuaji,51 wanahitaji mazoezi tiba (physiotherapy) na watoto 27 watakuwa
wakifuatiliwa kwa mwaka mmoja kabla ya kuanza matibabu.
Alisema watoto 36 ndio wamejitokeza awamu ya kwanza kufanyiwa upasuaji na wengine 17 watafanyiwa awamu nyingine lengo ni kuhakikisha watoto wanapatiwa huduma na kupona.
Bwasama ,alisema msaada huo pia unatokana na mchango kwa jamii unaotolewa na kampuni hiyo(SCR),kutokana na mapato yanayopatikana katika shughuli za utalii na uhifadhi.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri hiyo, Bonji Bugeni, wamepongeza msaada unaotolewa na Mwiba Holdings akisema umeleta faraja
kubwa kwa wazazi na watoto waliokosa uwezo wa kugharamia matibabu.
Bugeni alisema wazazi wa watoto hao sasa wameokolewa fedha na muda wa matibabu na hivyo, watarejea katika shughuli zao za uzalishaji mali na kupambana na umasikini.
Wazazi Neema Daniel na Angela Sai walishukuru msaada huo na kueleza watoto wao wanachangamoto ya matege ya ndani na wanaimani baada ya matibabu watarejea salama nyumbani.
Neema mkazi wa kijiji cha Makao alisema ameshindwa kugharamia matibabu ya mtoto wake kwani ni makubwa na sasa baada ya msaada huo anaamini mtoto wake atapona na kwenda shule kusoma sawa na watoto wengine.
Timotheo Ngassa, mkazi wa Kijiji cha Sapa, akizungumza kwa niaba ya wazazi, alisema mtoto wake Emmanuel ani miongoni mwa watoto28 waliofanyiwa upasuaji mwaka jana na sasa anaendelea vizuri alikuwa hatembei na sasa anatembea.
Ngassa alisema huduma ya Mwiba ni nzuri sana na aliomba huduma hiyo kutolewa wilaya nzima ya Meatu kwani kuna watoto wengi sana wanahitaji msaada wa matibabu na wazazi wao hawana uwezo kugharamia.
"Kwa niaba ya wazazi wengine tunawashukuru sana Mwiba kwa kugharamia upasuaji wa watoto mwaka jana na mwaka huu tunawaombea kwa Mungu wakurugenzi wa Mwiba na Friedkin kwa maono haya makubwa kusaidia jamii"alisema
Mwiba Holdings Ltd imewekeza wilayani Meatu katika Pori la Akiba la Maswa, Makao Ranch na hifadhi ya kijiji cha Mwangudo kwa shughuli za utalii wa picha na hoteli na imekuwa ikitoa misaada kadhaa kwa jamii, ikiwepo kujenga vituo vya afya, nyumba za walimu, vituo vya ulinzi kupambana na wanyama wakali, kugharamia chakula cha bure shuleni na misaada mingine kadhaa .

No comments: