LIVE STREAM ADS

Header Ads

DKT. NCHIMBI AFANYA MKUTANO MKUBWA KUNADI SERA ZA CCM SHINYANGA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

 

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwahutubia wananchi wa Shinyanga wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika leo Jumatano Septemba 3, 2025 katika Jimbo la Shinyanga Mjini.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi kumsikiliza Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Jumatano Septemba 3, 2025, Jimbo la Shinyanga Mjini.

Katika mkutano huo uliofurika umati wa wananchi, Dkt. Nchimbi amewanadi wagombea wa ubunge wa mkoa huo akiwemo Mhe. Patrobas Katambi (Shinyanga Mjini), Mhe. Lucy Mayenga (Kishapu), Mhe. Ahmed Salum (Solwa), na Mhe. Azza Hillal Hamad (Itwangi), pamoja na wagombea udiwani.

Dkt. Nchimbi amewaomba wananchi kumpigia kura za kishindo mgombea Urais wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wabunge na Madiwani wa chama hicho, akisisitiza kuwa kuchagua viongozi wote wa CCM kutaunda mnyonyoro thabiti wa uongozi utakaoharakisha maendeleo ya wananchi.
Akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030), Dkt. Nchimbi amesema imelenga kuboresha maisha ya wananchi katika sekta zote muhimu.

Ametaja miradi mipya itakayotekelezwa Jimbo la Shinyanga Mjini ikiwemo ujenzi wa Zahanati mpya 10, Vituo vya Afya 7 na Wodi 10 za wazazi. Sekta ya elimu itanufaika na shule mpya za msingi 7, madarasa 200, shule mpya za sekondari 6 na madarasa 288.

Katika sekta ya maji, ameahidi kuendelezwa kwa miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria na ujenzi wa visima virefu, huku sekta ya viwanda ikipewa kipaumbele kwa kujengwa viwanda vya ngozi na kuchenjua madini ili kuinua uchumi wa wananchi wa Shinyanga.

Aidha, akizungumzia mpango wa siku 100 za kwanza baada ya ushindi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Nchimbi amesema serikali itaajiri walimu 7,000 wa Sayansi na Hisabati, watumishi wa afya 5,000 na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 200 kwa wananchi.

Akirejea utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020–2025), amebainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana yakiwemo ongezeko la bajeti ya Wizara ya Afya kutoka shilingi bilioni 900 hadi trilioni 1.6.
Katika Jimbo la Shinyanga Mjini pekee, ametaja mafanikio ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Ibadakuli kwa kilomita 2.2, ongezeko la vituo vya afya kutoka 5 hadi 6, zahanati kutoka 44 hadi 59, pamoja na kuimarishwa huduma za afya kupitia vifaa vipya vya CT-SCAN na X-Ray Digital.

Vilevile, shule za msingi zimeongezeka kutoka 77 hadi 92, sekondari kutoka 44 hadi 49, huku visima virefu vya maji vikiongezeka kutoka 2,618 hadi 3,456.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Stephen Masele, amemkubali Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Patrobas Katambi, katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, kuwa ni mchapakazi na ameleta maendeleo makubwa jimboni humo, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Masele akizungumza mara baada ya kuagizwa na Dk.Nchimbi kumleta Mgombea Ubunge Katambi kwenye hadhara ili amnadi kwa wananchi, amesema Katambi ni kizazi kipya na amefanya maendeleo makubwa katika jimbo la Shinyanga kipindi cha miaka mitano iliyopita, hivyo anastahili kuugwa mkono na kuendelea kuwa Mbunge wa Jimbo hilo 2025-2030.

“Mimi ndiyo niliyemuachia Kijiti cha Ubunge Katambi katika Jimbo hili la Shinyanga Mjini, na kama mpira mimi nilikuwa napiga basi nyingi, lakini mwenzangu akapiga 'Counter Attack' na matobo mengi akafunga Goli,”amesema Masele.

“Katambi ni kizazi kipya amefanya maendeleo makubwa katika jimbo la Shinyanga Mjini,nitamuunga Mkono ili CCM ipate ushindi wa kishindo,na nitaendelea kumshauri kwa kushirikiana na wazee aendelee kuleta maendeleo hapa Shinyanga,”ameongeza Masele.
Aidha,amesema pamoja na kumuombea kura Katambi pia anawaombea kura madiwani wote wa CCM na kura nyingi kwa Mgombea Urais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi, ameeleza utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo barabara, masoko, stendi mpya ya mabasi na upanuzi wa uwanja wa ndege.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM umekuwa wa kiwango cha juu mkoani humo, na kusisitiza kuwa Shinyanga ni ngome ya CCM ambayo itashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwahutubia wananchi wa Shinyanga wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika leo Jumatano Septemba 3, 2025 katika Jimbo la Shinyanga Mjini.
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwahutubia wananchi wa Shinyanga wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika leo Jumatano Septemba 3, 2025 katika Jimbo la Shinyanga Mjini.





Elizabeth Maliganya alivyoamsha Shangwe Uzinduzi Kampeni za UCHAGUZI mkuu CCM Shinyanga

Saida Karoli akiamsha amsha Live uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 CCM Shinyanga

Ng'wana Kang'wa akishambulia JUKWAA uzinduzi wa Kampeni za uchaguzi Mkuu 2025 CCM Shinyanga Mjini

No comments:

Powered by Blogger.