Serikali kuimarisha usimamizi wa hifadhi ya mazingira ili kukabiliana na adha ya mafuriko
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kuboresha usimamizi wa hifadhi ya mazingira ili kuwaondolea wakazi wa Kilosa mkoani Morogoro na maeneo mengine adha ya mafuriko ya mara kwa mara.Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati alipopewa nafasi na Waziri Mkuu Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba awasalimie wakazi wa Tindiga wilayani Kilosa mkoani Morogoro
Januari 02, 2026 baada ya kukagua athari za mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Dkt. Dugange amesema tayari Serikali ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya imeshaanza utekelezaji wa mpango wa utunzaji wa mazingira kwa kusimamia zoezi la upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuongeza kasi ya upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kutokea kwa mafuriko.
Alitoa rai kwa halmashauri zote nchini kuweka utaratibu kuwa kila mwananchi kupanda miti angalau mitano kwa mwaka na kuitunza, hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Dkt. Dugange alielezea umuhimu wa upandaji miti na kubainisha kuwa maeneo yanapokosa miti ya kutosha, mvua inaponyesha husababisha mafuriko.
"Ukweli ni kwamba bado kasi ya upandaji wa miti inahitajika, mafuriko haya ndugu zangu Wana-Tindiga yanatokana na mito yetu kuwa na kina kifupi, mvua zikinyesha maji yanatapika yanakuja kwenye makazi ya wananchi na kuleta madhara makubwa, madhara ya kupoteza maisha, kuharibu miundombinu kwenye kilimo, kuharibu vituo vya huduma na makazi ya watu," alisema.
Pia, Dkt. Dugange alisema kuwa miongoni mwa nguzo zilizomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025-2050) ni Uhifadhi wa Mazingira na Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ambayo inahitaji nguvu za pamoja ili kufikia shabaha ya uboreshaji wa mazingira hasa kwa kupanda miti kwa wingi.
Katika salamu hizo, Mhe. Dkt. Dugange aliungana na Mhe. Waziri Mkuu kutoa pole kwa wananchi wa Tindiga na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla kutokana na madhara ya mafuriko yaliyotokea.
No comments: