WAZIRI MKUU AZINDUA MELI MPYA YA MV NEW MWANZA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amezindua rasmi meli mpya ya kisasa ya MV New Mwanza, iliyojengwa na Mkandarasi Gas Entec Ship- Building kutoka Korea kwa gharama ya Tshs. Bilioni 120.56.
Akizungumza Ijumaa Januari 24, 2026 jijini Mwanza na wananchi katika eneo la Bandari ya Mwanza Kusini, Dkt. Mwigulu alisem ujenzi wa meli hiyo ya kisasa ni ishara ya juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuhakikisha wanamaliza kiu ya kuwa na usafiri imara katika ziwa Victoria.
Pia alitumia fursa hiyo kuagiza Wizara ya Uchukuzi kuendeleza ujuzi uliotumika kujenga meli hiyo, huku shirika la meli nchini TASHICO likishirikiana na wadau wengine kulinda mradi huo kwa kuweka bima na kufuata ushauri wa kitaalamu na kuimarisha na kukuza diplomasia ya mahusiano na amani.
Alitoa maelekezo pia kwa wizara zinazosimamia miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu kufanya tathmini kubaini miradi ambayo wakandarasi hawajalipwa fedha ili walipwe na ikamilike kama mradi huo wa meli na kuleta tija kwa jamii.
"Mawaziri wa kisekta, fanyeni tathmini kwenye miradi yote ambayo mikataba imeshasainiwa lakini wakandarasi hawajapata fedha za awali na wizara ya fedha pitieni mafungu yote isipokuwa ya vyombo vya usalama na Afya mkate mpeleke fedha kwenye miradi hii ili ikamilike" alisema Dkt. Mwigulu.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani ilikuta meli hiyo imejengwa kwa asilimia 40, zikiwa zimelipwa kiasi cha shilingi bilioni 40.64 na hivyo kutoa shukurani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa shilingi bilioni 79.98 na kuwezesha mradi huo kukamilika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisema kukamilika kwa meli hiyo kutaboresha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kupunguza adha ya usafiri kati ya Mwanza na Bukoba pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.



No comments: