WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI MWANZA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na maatenki ya kuhifadhia maji unaotekelezwa katika mtaa wa Sahwa, Kata ya Lwahnima jijini Mwanza.
Akizungumza Ijumaa Januari 23, 2026 katika hafla hiyo fupi ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi huo unaotoa maji chanzo cha Butimba, Dkt. Mwigulu aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa haraka kwa lengo la kuondoa kero ya maji kwa wananchi, akisisitiza kuwa serikali itakua macho kuwasimamia.
Pia Dkt. Mwigulu alitoa maagizo maagizo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha kuwa fedha za zinazotoka kwaajili ya miradi ya maji zinakwenda kwenye miradi kwa haraka kwa sababu maji kama huduma ya kijamnii haina mbadala kwa wananchi kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alisema atashirikiana na Katibu Mkuu wa wizara yake kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi ili mradi uweze kukamilika ndani ya muda kama mkataba unavyosema.
Awali akisoma taarifa ya mradi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), Nelly Msuya alisema mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi SINOHYDRO CORPORATION LIMITED & HIGHLAND BUILD CO., LTD (JV) ni sehemu ya programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria (LVWATSAN), yenye lengo la kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi pamoja na usafi wa mazingira kwa Jiji la Mwanza na maeneo jirani.
Alibainisha mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya 450,000 jijini Mwanza, Magu na Misungwi katika maeneo ya Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyamazobe, Nyahingi, Buganda, Luchelele, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri na Igoma. Katika Wilaya za Magu na Misungwi mradi utanufaisha wakazi wa Kisesa, Bujora, Kanyama, Fela na Usagara kwa kupata huduma ya maji safi na ya uhakika, jambo ambalo litachangia kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji machafu.
Mradi huo ulianza rasmi kutekelezwa mwezi Juni, 2024 na unatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2026 huku gharama za utekelezaji wa mradi huo ni zaidi ya Tsh. bilioni 46.
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Nelly Msuya akitoa ufafanuzi kwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.



No comments: