RC MWANZA ASISITIZA UJENZI SHULE YA MSINGI AMALI KISHIRI UKAMILIKE
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akiweka (mwenye kofia) akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Amali Kishiri jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesisitiza ujenzi shule mpya ya msingi ya Amali Kishiri jijini Mwanza, ukamilike kwa haraka ili watoto waanze kupata elimu bora katika mazingira rafiki na salama.
Msisitizo huo aliutoa Alhamis Feburuari 12, 2026 baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo uliopo katika kata ya Kishiri jijini Mwanza.
Alisema shule za Amali zinajengwa ili watoto wapate mafunzo ya ufundi kuanzia darasa la awali hatua itakayosaidia taifa kupata wataalamu mbalimbali wakiwemo mafundi nyumba, umeme na rangi.
"Mtoto anapoanza kujifunza kitu tangu anapokuwa mdogo inamsaidia kuelewa vizuri na kutunza kumbukumbu ya kile alichofundishwa hivyo shule hizi za Amali zitakwenda kusaidia watoto wengi kuwa na uwezo wa kujiajiri pindi wanapokuwa wamemaliza elimu ya sekondari na vyuo" alisema Mtanda.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igoma ambaye ni msimamizi wa ujenzi huo, Anthony Masanja alisema mradi huo hadi kukamilika utagharimu shilingi milioni 330.7
Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Novemba 12, 2025 na ulikusudiwa kukamilika Feburuari 13, 2026 ambapo ameeleza kuwa mkandarasi ameomba kuongezewa muda wa wiki tatu ili aweze kumalizia ujenzi huo.
Aidha alisema mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kupunguza mrundikano wa wanafunzi kwa shule jirani za msingi ambazo ni Kishiri, Shamaliwa na Uhuru.
Pius Joseph na Martha William ambao ni baadhi ya wakazi wa Kishiri waliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna inavyoendelea kutekeleza miradi ya elimu huku wakiongeza kuwa uwepo wa shule hiyo itawasaidia kujua vipaji vya watoto wao mapema.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Baadhi ya wananchi na viongozi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Amali Kishiri jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akiwa na viongozi wengine katika ukaguzi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Amali Kishiri jijini Mwanza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igoma ambaye ni msimazi wa shule ya msingi Amali Kishiri, Mwl Antony Masanja akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo.




No comments: