LIVE STREAM ADS

Header Ads

ALICHOKISEMA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII WAKATI AKIWAKABIDHI TUZO WASHINDI WA HABARI ZA TANAPA MWAKA 2013/14.


Mh.Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mh.Lazaro Nyalandu amebainisha kuwa Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa ya kulisaidia Taifa, katika kukabiliana na changamoto za Ujangili ambazo zinalikabili Taifa na kuhatarisha hali ya Utalii katika hifadhi mbalimbali hapa nchini.
 
Mh.Nyalandu aliyasema hayo jumanne ya wiki hii May 27 Mkoani Mwanza, katika hafla ya kuwakabidhi tuzo washindi wa Tuzo za Shirika la Hifadhi za Taifa nchini TANAPA mwaka 2013/14 zinazohusiana na Uandishi wa Makala za Utalii kupitia Radio, Luninga na Magazeti.

Alisema Waandishi wanapozishika kalamu zao wajue wanaifanya kazi ya Watanzania, hivyo waifanye kazi hiyo kwa uhuru mkubwa, huku akibainisha kwamba habari watakazoziandika juu ya kupambana na Ujangili zitasaidia kuinua hali ya Utalii hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuwaandika wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya ujangili.

Zaidi aliwasisitia wanahabari kwamba wanapaswa Kuifanya kazi ya kuielimisha jamii kupitia habari zinazohusiana na vivutio pamoja na hifadhi mbalimbali za Utalii hapa nchini ili kuwafanya wananchi wa kawaida kupenda raslimali za nchi yao.

Aidha alibainisha kwamba katika mwaka wa 2014/15 ameandaa mpango maalumu wa Kuhuiisha Mtazamo wa Tanzania katikaki ya Mataifa na kuifanya Tanzania kuondokana na hali ya kulalamika bali kuifanya dunia ishangazwe na Tanzania hali ambayo pia itabadilisha idadi ya watalii nchini hadi kufikia watalii Milioni Mbili mwaka 2015/17 kutoka watalii Milioni 1.1 kwa mwaka 2012/13.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini TANAPA, Alan Kijazi aliwataka waandishi wa habari kuwa na Umoja katika kufanya kazi zinazohusiana na utalii kwa kuwa TANAPA iko tayari kuwasaidia waandishi wa habari kupitia umoja wao.

Alisema kwa sasa TANAPA inashindwa kuwasaidia waandishi wa habari wanaoandika habari za utalii kupitia vyama vyao, na hivyo kuwasihi waandishi wa habari za Utalii kuwa na Chama kimoja ambacho TANAPA inaweza kushirikiana nacho katika uandishi wa habari za Uhifadhi na Utalii, huku akiweka wazi kwamba TANAPA iko tayari kusimamia mafunzo ya Uandishi wa habari za Uhifadhi na Utalii kwa wanahabari.
 
KUHUSU TUZO ZA TANAPA


Nazo Tuzo za TANAPA mwaka 2013/14 ziligawanyika katika Makundi mawili ambapo kulikuwa na kundi la kwanza ambalo lilikuwa linahusiana na Makala zinazohusiana na Utalii wa Ndani, pamoja na kundi la pili ambalo lilikuwa linahusu Masuala ya Uhifadhi. Ambapo katika Tuzo hizo kulikuwa na washindi watatu kutoka katika kila mgawanyo wa vyombo vya habari ambavyo ni Radio, Luninga na Magazeti ama Mitandao ya Kijamii (Blogs).
 
Katika Tuzo hizo Mshindi wa Kwanza alijinyakulia Hundi ya Shilingi Milioni mbili, cheti, ngao pamoja na Safari ya Kimafunzo katika mojawapo ya nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, na Mshindi wa Pili akijipatia Hundi ya Shilingi Milioni moja na nusu, cheti pamoja na safari ya kimafunzo katika hifadhi mbili za Kitaifa hapa nchini, huku mshindi wa tatu akijipatia Hundi ya Shilingi Milioni moja pamoja na cheti. Zawadi hizo zikiwa ni linganifu kwa washindi wa Radio, Luninga na Magazeti.

Washindi wa Tuzo za TANAPA 2013/14 kundi la Utalii wa ndani

Upande wa Magazeti mshindi wa kwanza alikuwa ni Gerald Kitabu kutoka The Guardian, mshindi wa pili Frank Leornad kutoka Habari leo na Mshindi wa tatu Jackson Kalindimya kutoka gazeti la Nipashe. Upande wa Radio Mshindi wa Kwanza alikuwa ni David Rwenyagila kutoka Radio Five, Mshindi wa Pili Hamphrey Mgonja Kutoka Radio Saut huku mshindi wa tatu akishindwa kupatikana. Na kwa Upande wa Luninga Mshindi wa Kwanza pia hakuweza kupatikana, Mshindi wa pili alikuwa ni Cacius Mdame wa Chanel Ten na Mshindi wa Tatu alikuwa ni Kakuru Msimu kutoka Star Tv.
 
Washindi wa Tuzo za TANAPA 2013/14 kundi la Masuala ya Uhifadhi

Upande wa Magazeti mshindi wa kwanza na wa Pili hawakuweza kupatikana kutokana na kutofikia vigezo vya majaji, Mshindi wa Tatu alikuwa ni Salome Kitomali kutoka Nipashe. Upande wa Radio Mshindi wa Kwanza pia hakuweza kupatikana, Mshindi wa Pili alikuwa ni David Rwenyagila huku mshindi wa Tatu pia akishindwa kupatikana. Na upande wa Luninga Mshindi wa Kwanza alikuwa ni Vedasto Msungu kutoka ITV, Mshindi Wa Pili Raymond Nyamwihula wa Star TV ambapo mshindi wa Tatu upande wa Luninga pia hakuweza kupatikana.

Kwa mjibu wa Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Tuzo hizo za TANAPA 2013/14 Dk.Ayub Rioba ambae ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Kwamba nafasi ambazo washindi hawakupatikana zilitokana na Jopo la majaji kutoridhika na makala zilizowasilishwa kulingana na vigezo vilivyokuwa vimewekwa. Ambapo miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na Makala kutokuwa na udhamni wa aina yoyote kutoka TANAPA, kuwa na uthibitisho kutoka kwa Mhariri wa chombo husika, na iwe haijawahi kutumwa katika tuzo zilizopita sanjari na kuwa imetumika katika kipindi cha kati ya mwezi wa Kwanza hadi mwezi wa 12 mwaka uliopita.

No comments:

Powered by Blogger.