LIVE STREAM ADS

Header Ads

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII AZINDUA MPANGO WA NYOTA YA KIJANI MKOANI MWANZA.


Picha haihusiana na Uzinduzi
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Kebwe Steven Kebwe amebainisha kuwa katika bajeti ijayo Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni Tatu, kwa ajili ya Kusaidia upatikanaji wa Huduma bora za Uzazi wa Mpango hapa nchini.

Dkt.Kebwe alitoa kauli hiyo hii leo Mkoani Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana wakati akizindua Mpango wa Nyota ya Kijani katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mpango ambao umelenga kuhamasisha wananchi kutumia huduma za Uzazi wa Mpango sanjari na kusogeza karibu huduma hizo kwa wananchi hususani walioko vijijini.


Alibainisha kwamba matumizi ya Uzazi wa Mpango hapa nchini yako katika kiwango cha chini ukilinganisha na nchi nyingine duniani, ambapo Kitaifa Matumizi ya Uzazi wa Mpango yako chini ya asilimia 27 ikilinganishwa na nchi zilizoendelea ambazo zimefikia kiwango cha zaidi ya asilimia 70.

Aidha Dkt.Kebwe aliwashukuru wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambayo wanasaidia katika kuboresha huduma za Uzazi wa Mpango hapa nchini, ikiwemo Shirika la Afya Ulimwenguni kwa kusaidiana na Shirika la Idadi ya Watu duniani ambayo yamesaidia Shilingi Bilioni Sita kwa ajili ya Kusaidia kuboresha huduma za uzazi wa Mpango hapa nchini.


Akitoa taarifa ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juu ya tathimini ya Kiwango cha Utumiaji wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto ambayo inajumuisha huduma ya Uzazi wa Mpango hapa nchini, Helem Semu ambae ni Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha elimu ya Afya kwa Umma, amebainisha kuwa kiwango cha utumiaji wa Uzazi wa Mpango katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi kiko chini ukulinganisha na Mikoa ya Kasikazini.


“Katika Mkoa wa Mwanza ambao uko Kanda ya Ziwa kiwango cha utumiaji wa Mpango wa Uzazi kiko chini ya asilimia 12, ukilinganisha na kiwango cha asilimia 50 katika Mkoa wa Kilimanjaro ulioko Kanda ya Kasikazini”,  huku akibainisha kuwa “Wizara inafanya jitihada ili kuongeza kiwango cha utumiaji wa uzazi wa Mpango katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi”.Akisema Semu.


Nao baadhi watumiaji wa Huduma ya Uzazi wa Mpango waliwahimiza wanajamii wengine ambao hawajajiunga na mpango wa Uzazi wa Mpango kuchukua maamuzi ya kujiunga kwa kuwa njia za uzazi wa mpango hazina madhara yoyote mbali na kuwa na faida mbalimbali ikiwemo kupanga familia bora.


Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Valetino Bangi aliwahimiza wananchi kutumia huduma za uzazi wa mpango, ambapo wataweza kunufaika na faida mbalimbali zitokanazo na mpango huo ambazo ni pamoja na kupunguza vifo vya watoto sanjari na akina mama kutokana na ujauzito na uzazi.


Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mh.Baraka Konisaga alisisitiza juu ya upatikanaji wa huduma bora za Uzazi wa Mpango kwa kuwa uzazi wa Mpango unaweza kusaidia kupunguza vifo vya uzazi hadi kufikia asilimia 44.

No comments:

Powered by Blogger.