LIVE STREAM ADS

Header Ads

UZINDUZI WA NYOTA YA KIJANI KWA MIKOA YA KANDA YA ZIWA KUFANYIKA MKOANI MWANZA, NAIBU WAZIRI WA AFYA KUWA MGENI RASMI.



Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Kushirikiana na Wadau wa Afya ya Uzazi inazindua upya Kampeni ya Nyota ya Kijani katika Mikoa Mitano ya Kanda ya Ziwa, ambapo uzinduzi huo unatarajia kufanyika kesho jumanne May 20, 2014 katika Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
 
Akitoa taarifa ya Uzinduzi huo hii leo kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mh.Baraka Konisaga alibainisha kwamba, Uzinduzi huo ni sehemu ya Mkakati wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikiana na Asasi zinazotoa huduma za Uzazi na Mtoto kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema lengo la Mpango huo wa Nyota ya Kijani ni Kuongeza Kiwango cha Upatikanaji na Matumizi ya Huduma ya Uzazi wa Mpango katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha Utumiaji wa Uzazi wa Mpango katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa iko katika kiwango cha chini.
Mikoa inayo inayohusika na Uzinduzi huo ni Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, na Geita ambayo wastani wakw wa matumizi ya njia za kisasa za Uzazi wa Mpango ni chini ya asilimia 13 ikilinganishwa na wastani wa Kitaifa wa Asilimia 27.

Kwa mantiki hiyo Konisaga alibainisha kwamba kampeni hiyo ya Nyota ya Kijani ni kampeni maalumu ambayo imelenga kuhamasisha wananchi kutumia huduma za uzazi wa mpango sanjari na kusogeza huduma za uzazi wa mpango kwa wananchi hususani walio vijijini.

“Uzinduzi wa Nyota ya Kijani Kitaifa ulifanyika Oktoba 11 mwaka jana na Makamu wa Rais Dkt.Mohamed Gharib Bilal katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam, alipotangaza nia ya Serikali ya Kuimarisha huduma za uzazi wa Mpango ili kufikia ahadi ya Mh.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufikia kiwango cha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango cha asilimia 60 ifikapo mwaka 2015”.Alisema Konisaga.

Kufuatia mwamko wa wananchi kutumia uzazi wa Mpango kuwa chini katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mganga Mkuu wa Mwanza  Dkt.Valentino Bangi alibainisha kuwa ni kutokana na wananchi wake kuwa na imani tofauti tofauti ikiwemo wazazi kuamini kwamba kuzaa watoto wengi katika familia kunaleta manufaa mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi.

Hata hivyo Dkt.Bangi alitoa rai kwa wananchi kuzingatia Mpango wa Nyota ya Kijani ambao umelenga kuwahimiza wananchi kutumia mpango wa uzazi sanjari na kuboresha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.

Miongoni mwa faida za uzazi wa Mpango ni pamoja na kuokoa maisha ya akina mama wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua kwa wastani wa asilimia 40, huku ukisaidia kupunguza vifo vya watoto wadogo wachanga.

Naibu waziri wa Afya Mh.Kebwe Steven Kebwe anatarajiwa kuzindua mpango huo wa Nyota ya Kijani kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa hiyo kesho katika Uwanja wa Nyamagana ambapo huduma mbalimbali za uzazi wa mpango zitatolewa huku zikitanguliwa na maandamano yatakayoanzia katika Hospital ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure kuanzia majira ya saa mbili za asubuhi.

No comments:

Powered by Blogger.