ZAIDI YA WASICHANA 3,000 WAKO HATARINI KUKEKETWA WILAYANI TARIME, MKOANI MARA. HATUA ZAIDI ZINAPASWA KUCHUKULIWA.
![]() | ||
Namna shughuli ya ukeketaji inavyofanyika |
Hayo
yamebainishwa mwishoni mwa mwaka jana Wilayani humo na moja wa Wazee wa Kimila kutoka
katika kabila la wakurya katika koo ya Watimbaru, wakati akizungumza na
mwandishi wa habari hizi aliefika Wilayani humo kuangazia juhudi za kupambana na vitendo vya ukeketaji
kwa wasichana.
Pamoja na idadi hiyo bado kuwa kubwa lakini Mzee huyo anaefahamika kwa jina la Mwikwabe Mwita Masero, alieleza kwamba idadi ya wasichana wanaofanyiwa ukeketaji kwa miaka ya hivi karibuni inazidi kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma, japo hakutaja idadi hiyo imepungua kwa kiasi gani.
Mzee huyo
alifafanua kuwa katika msimu wa ukeketaji ambao hufanyika mara moja kwa mwaka,
kila baada ya miaka miwili, idadi ya wasichana wanaofanyiwa ukeketaji
inakadiriwa kufikia kati ya elfu tatu hadi elfu nne kwa koo moja, idadi ambayo
aliitolea mfano kwa koo ya moja ya watimbaru, ambapo itakumbukwa kuwa kabila la
wakurya linaundwa na jumla ya koo 13 na zote zikiwa zinatekeleza mila hiyo japo
kila moja katika nyakati tofauti.
“Idadi, aaaah mfano katika koo ya watimbaru
wanaweza kufika kama elfu tatu au elfu nne hivi kwa msimu,” alisema mzee huyo
tena bila mshangao wowote kulingana na idadi hiyo jinsi ilivyokubwa.
![]() |
huu ni ukatili (msichana akikeketwa) |
Baadhi ya wananchi Wilayani Tarime walieleza
kwamba, pamoja na mwitikio wa utekelezaji wa mila hii kuanza kupungua japo kwa
kiasi kidogo sana kwa baadhi ya maeneo Wilayani humo, kutokana na juhudi za
mashirika na taasisi mbalimbali kuanza kutoa elimu ya kupambana na ukeketaji,
bado elimu hiyo haijawafikia vyema watu wote hususani wazee wa kimila na
mangariba, na hivyo kuna haja ya jambo hilo kutiliwa mkazo zaidi.
Akiwa ni miongoni mwa wanainchi wachache waliobahatika kupata elimu ya kupiga vita masuala ya ukeketaji Wilayani Tarime kutoka katika shirika la Pact Tanzani ambalo limekuwa likiendesha semna na mafunzo mbalimbali kwa wananchi wa Wilaya ya Tarime, Zephania Mwita Mang’ache anasema kwamba amebadilika sana kimtizamo na ametokea kuichukia mila hiyo ya ukeketaji.
“Mimi hii
elimu ya kupambana na ukeketaji nimebahatika kuipata katika NGO’s moja hivi
inayoitwa Pact; kiukweli Pact wamenisaidia sana kupata uelewa wa masuala haya
ya ukeketaji, hivyo ningeshauri na mashirika mengine yaanze kutoa ulimu kama
hii hapa Wilayani hususani kwa wazee wa kimila na mangariba kwa kuwa wao ndio
wanaosimamia zoezi hili la ukeketaji” alisema.
![]() |
ukeketaji haukubaliki |
Itakumbukwa
kuwa Mila na desturi hii ya ukeketaji inaendelea kupigwa vita hasa kutokana na
madhara yake kwa msichana/mwanamke aliekeketwa, madhara ambayo ni pamoja na
binti kupoteza damu nyingi wakati na baada ya ukeketaji, kupata madhara ya
kiafya ikiwemo wakati wa kujifungua na wakati mwingine kupoteza maisha sanjari
na kupata maumivu makali wakati wa ukeketaji na mengine mengi.
Jambo la kusikitisha ni kwamba idadi hiyo bado ni kubwa sana na inatishia mbaya zaidi idadi hiyo ni ya koo moja ya kabila la Wakurya, ambapo itakumbukwa kuwa kabila la wakurya linaundwa na jumla ya koo 13 na zote zinatekeleza mila hiyo japo kila moja katika kipindi tofauti, ambapo kwa koo ya Watimbaru wanatarajia kufanya ukeketaji mwezi wa 12 mwaka huu.
Ukweli ni kwamba elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa wazee wa kimila, mangariba sanjari na jamii nzima kwa ushirikiano wa karibu kabisa na serikali pamoja na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika na taasisi binafsi ili kuweza kuwaokoa wasichana hawa kutoka katika janga hili la ukeketaji.
USIKOSE KUFUATILIA MAKALA JUU YA UKEKETAJI WILAYANI TARIME KATIKA BLOG HII, KWA USHAURI NA MAONI TUWASILIANE KUPITIA 0757 43 26 94.
No comments: