LIVE STREAM ADS

Header Ads

UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI KUFANYIKA KESHO, JIJI LA MWANZA KUWA MWENYEJI WA MAADHIMISHO HAYO KITAIFA. SOMA ALICHOKISEMA MTUMISHI WA MUNGU KUHUSIANA NA MAADHIMISHO HAYO.


Konisaga (Mtumishi wa Mungu)
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yanatarajiwa kufunguliwa kesho June 02 na kufikia kilele chake June 05 mwaka huu, ambapo Mkoa wa Mwanza umeteuliwa kuwa mwenyeji wa Maadhimisho hayo Kitaifa.
 
Katika Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo iliyosomwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga (Mtumishi wa Mungu) ambae anakaimu Ofisi yake, ilieleza kwamba Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufunguliwa kesho katika Uwanja wa Furahisha Mkoani Mwanza na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt.Binilith Mahenge.

Taarifa hiyo ilibainisha kwamba katika juma la Maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo yote, kuhamasisha wananchi kuhusiana na utunzaji wa mazingira kwa njia ya makongamano.

Shughuli nyinge ni kupanda miti, kuzoa takataka, maonyesho ya utunzaji wa mazingira, kuondoa magugu maji katika ziwa Victoria, ufugaji wa nyuki pamoja na kufanya ziara katika maeneo yanayojishughulisha na utunzaji wa mazingira ikiwemo viwanda.

Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika June Tano Mwaka huu, anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dkt.Mohamed Gharib Bilal ambae anatarajiwa kukabidhi vyeti kwa wadau mbalimbali wa mazingira, zawadi na tuzo ya Rais ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira pamoja na zawadi nyinginezo kwa washindi wa Uhifadhi wa Mazingira.

“Natambua kwamba ninyi ni wadau wakubwa sana wa Mazingira hasa katika jukumu lenu la kuelimisha umma, juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, kwa nafasi ya pekee niwaombe muweze kuipeleka taarifa hii kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani ili waweze kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Furahisha kwa muda wote ambao elimu kuhusu utunzaji wa mazingira itakuwa ikitolewa na wadau mbalimbali” Alisema Konisaga wakati akizungumza na wanahabari.

Aidha Konisaga alihitimisha kwa kwa kutoa rai kwa wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi na kushirikiana na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi watakaofika Jijini Mwanza kwa ajili ya Maadhimisho hayo kwa kuonyesha ukarimu wa hali ya juu kama ilivyo ada ya wanamwanza, sanjari na kuwahimiza kuzingatia usafi katika maeneo yao ili kuwezesha Jiji la Mwanza kuendelea kuwa Jiji Safi katika Mashindano ya Majiji hapa nchini.
Konisaga Kushoto, Kulia ni Madete
Angelina Madete
Tayari Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Angelina Madete yuko Mkoani Mwanza kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira duniani, ambapo katika Maelezo yake alieleza kwamba siku hii inakumbusha juu ya umhimu wa kutunza mazingira katika maisha kwa kuzingatia uzalishajimali ambao hauathiri uhifadhi na utunzaji wa Mazingira. 

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo Kimataifa ni “Chukua Hatua Kukabiliana na Mabadiliko” ambapo Kitaifa ni “Tunza Mazingira ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” zote zikiwa mahsusi kwa ajili ya kuhimiza juu ya umuhimu wa Uhifadhi wa Mazingira.

No comments:

Powered by Blogger.