LIVE STREAM ADS

Header Ads

MUHIMU KUTOKA HIFADHI YA TAIFA SAANANE ILIYOKO MKOANI MWANZA.



Hifadhi ya Saanane iliyoko Mkoani Mwanza ilianzishwa kama bustani ya kwanza ya wanyama hapa nchini mwaka 1964 ambapo lengo la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kuhamasisha Uhifadhi na Kuelimisha jamii katika masuala ya Uhifadhi na Utalii.

Chimbuko la jina hilo (Saanane) lilitokana na mwanzilishi wa bustani hiyo ya wanyama ambae alikuwa mwenyeji na Mkazi wa Kisiwa cha Saanane alieitwa Saanane Chawandi ambae hatimae alihamishwa katika Kisiwa hicho na Serikali na kupewa eneo jingine kwa ajili ya makazi yake.

Katika ya Mwaka 1964 na 1966 wanyama mbalimbali walihamishiwa katika kisiwa hicho, wanyama ambao ni pamoja na Mbogo, digidigi, tembo, pofu, pundamilia, pongo, swala pala, ngiri, kima, twiga, nungunungu, mamba sanjari na wanyama wengineo.

Mwaka 1991 bustani hii ya wanyama ya Saanane iligeuzwa kuwa pori la akiba (Game Reserve) na hatimae kulingana na umuhimu wake serikali ilikubali na kuanza mchakato wa kulipandisha hadhi pori hilo ili kuwa hifadhi ya Taifa, ambapo mwaka 2006 pori hilo lilikabidhiwa kwa TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa nchini) na hatimae Julai 2013 eneo la Saanane likatambuliwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Bi.Nkwambi anasema kuwa Umuhimu wa eneo la Saanane ambao ulichochea kugeuzwa kuwa Hifadhi ya Taifa ni pamoja na umuhimu wake kwa mazalia ya viumbe wa majini hususani Samaki aina ya Tilapia na Sato, lakini pia mamba pamoja na wanyama jamii ya Fisi Maji.

“Lakini pia eneo hili lina umuhimu mkubwa kwa jiji la mwanza na Taifa kwa ujumla kwa ajili ya kutoa elimu ya uhifadhi wa maliasili na mazingira kwa wakazi wa jiji la Mwanza, Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla hivyo ni eneo mahususi kwa ajili ya kufanya utafiti wa kisayansi ambapo wanafunzi wa ngazi mbalimbali hufika katika eneo hilo kwa ajili ya tafiti na kujifunza”.

Hifadhi hii ya Saanane ina eneo la kilomita za mraba 0.5 na iko umbali wa kilomita 2 kutoka kusini magharibi kutoka katikati ya jiji la Mwanza, katika ghuba ya Ziwa Victoria huku eneo la hifadhi hiyo likiwa linakamilishwa na visiwa viwili ambavyo ni Chankende kubwa na Chankende ndogo na hivyo kufanya ukubwa wa Hifadhi ya Saanane kuwa kilomita za mraba 2.18.

Tofauti na hifadhi nyingine, hifadhi ya Saanane ina wanyama ambao wameachiwa tofauti na wale waliofungiwa na hawana madhara yoyote kwa watalii ambapo katika hifadhi hiyo shughuli kubwa za utalii zinazofanyika ni matembezi kwa ajili ya kujionea mandhari nzuri ya hifadhi hiyo.

Lakini pia shughuli nyingine ni pamoja na kuangalia wanyama, kukwea miamba, kutizama ndege, kupiga makasia kutumia boti katika maji ya Ziwa Victoria katika maeneo yanayoizunguka hifadhi hiyo huku jambo la kufurahisha likiwa ni kufikika kirahisi muda na wakati wowote wa mwaka katika hifadhi hiyo ya Saanane.

Waongoza Watalii wakitoa maelekezo wa wahariri/ wanahabari walipofanya ziara kwa ajili ya utalii wa ndani katika hifadhi hiyo.Ziara kwa hisani ya TANAPA.
Wanahabari kazini katika hifadhi hiyo.Ilikuwa May 28 Mwaka huu kwa ushirikiano na TANAPA.
Afua Hamis ni Mwongoza watalii katika Hifadhi ya Saanane, yeye anasema kuwa eneo la Hifadhi ya Saanane ni eneo zuri kwa ajili ya pikiniki, kupumzika na kupiga picha za aina mbalimbali huku akibainisha kuwa ukiwa katika kisiwa hicho unapata fursa nzuri ya kulitizama Ziwa Victoria kwa mwonekano mzuri zaidi.

“Gharama za kutembelea katika hifadhi hiyo ya Saanane ni shilingi 5,000 kwa walio na umri kuanzia miaka 16 na kuendelea, Shilingi 2,000 kwa walio na umri kati ya miaka mitano na 16, huku walio na umri wa chini ya Miaka Mitano wakiwa wanaruhusiwa kuingia bure” Anasema na kuongeza:

“Aidha kwa Safari za kwenda na kurudi katika hifadhi hiyo ni Shilingi 35,000, kufanya utalii katika Maji ya Ziwa Victoria yanayozunguka Hifadhi hiyo kwa saa moja ikiwa ni shilingi 160,300 huku nusu saa ikiwa ni shilingi 80,150 ambapo boti hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 20 ambapo watalii wanaweza kulipia gharama hizo kwa kuchangia kila mmoja gharama isiyozidi shilingi 7,000”Anasema Afua.

Changamoto kubwa inayoikumba hifadhi hiyo ya saanane ni juu ya Uvuvi haramu kutokana na eneo linaloizunguka hifadhi hiyo kuwa na samaki wengi.Katika eneo hilo kuna changamoto ya wavuvi kutumia sumu kwa ajili kuvulia samaki jambo ambalo linahatarisha mazalia ya samaki.Hivyo kutokana na hali hiyo walinzi wanaoshika doria katika hifadhi hiyo wanazidi kujiimarisha ili kuhakikisha wanapambana na hali hiyo sanjari na kuimarisha ulinzi kwa ujumla katika hifadhi hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.