AFYA ZA WATUMIAJI MAJI ZIWA VICTORIA HATARINI...HII NI KUTOKANA NA UTIRIRISHAJI WA VINYESI KWENYE MITO INAYOMWAGA MAJI YAKE KATIKA ZIWA HILO.
![]() |
Usafi ukiendelea |
Hayo yalibainishwa
jana na baadhi ya wadau wa mazingira kutoka Ofisi za Maji Bonde la Ziwa
Victoria, Maafisa wa Afya wa Jiji la Mwanza na Jumuia ya Watumiaji wa Maji na
Utunzaji wa Mazingira walipokuwa wakifanya usafi Katika Mto huo ikiwa ni sehemu
ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani ambayo inafikia kilele chake June
Tano Mwaka huu.
Kaimu Afisa
wa Maji kutoka Bonde la Ziwa Victoria Godfrey Kajanja alisema kwamba, Ofisi
yake na Halmashauri ya Jiji zitakutana kuchukua hatua za kisheria kwa Kaya hizo
na watu walio na tabia ya kuchafua maji ya mito ikiwemo Mto Mirongo.
Kajanja
alisema kwamba, hali hiyo ikiachwa kuendelea bila kudhibitiwa kutawezesha
kuibuka magonjwa ya kuambukiza ikiwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoani Mwanza haitachukua hatua za kuongeza kiasi
kikubwa cha dawa ya kutibu maji kabla ya kusambazwa kwa watumiaji.
“Lazima sasa
tushirikiane kuzitekeleza sheria zilizopo za Mipango miji kwa upande wa Jiji la
Mwanza, pamoja na ofisi yetu ya Bonde kutumia sheria ya usimamizi wa rasilimali
ya maji Na. 11/2009 na sheria ya usimamizi wa mazingira Na. 24/2004 ambazo
zinaoanisha adhabu ya fedha na kifungo kwa watu watakaokaidi na kukutwa na
makosa,” alisema.
Kwa upande
wake Mhandisi wa Maji toka ofisi za Bonde la Ziwa Victoria Mhandisi Jane John
alieleza kwamba, hatua hivyo inatakiwa kukomeshwa mara moja na jamii iliyo
kandokando ya maeneo unapipita mto Miringo na maeneo ya vyanzo vya maji ili
kusaidia kulinda na tabia ya uchafuzi wa mazingira ikiwemo udhibiti jambo
ambalo litaepusha uharibifu na uchafuzi.
“Tumeshuhudia
mabomba ya vinyesi na maji machafu yakimwaga mtoni wakati tukifanya usafi wa
pamoja kwenye mto Mirongo na wadau mbalimbali walioko kwenye maadhimisho ya
siku ya mazingira kitaifa hili ni jambo ambalo linahitaji hatua za haraka
kulikomesha na kuwachukulia hatua wanaofanya uchafuzi huu,”alisisitiza.
Naye
Mwenyekiti wa NGO ya Jumuiya ya watumiaji maji na mazingira Adam Shija ya Kata
ya Mbugani Wilayani Nyamagana mkoani hapa alisema kwamba, tumekuwa na
changamoto kubwa wakati wa usafishaji wa mto huo na wamebaini kuwepo kwa baadhi
ya Kaya 75 ambazo zimekuwa zikitirilisha uchafu wa vinyesi na majimachafu ndani
ya mabomba yaliyoelekezwa mtoni humo.
Shija
alifafanua walipotembelea kandokando ya mto huo kwenye maeneo ya unapoanzia na
kupitia kasha kumwaga maji ziwani Victoria katika Kata za Nyakato walibaini
kaya 16, Mahina kaya 8, Mbugani kaya 24, Mirongo kaya 17, Nyamagana kaya 6 na
Pamba kaya 4 na tayari orodha hiyo imetokana na ukaguzi wa Jumuiya hiyo hivi
karibuni.
“Wito wangu
kwa Serikali na Idara zenye jukumu la kusimamia rasilimali ya maji na mito,
mabwawa na ziwa Victoria kutekeleza sheria kwa vitendo ili kukomesha tabia hii
ya uchafuzi wa maji na uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa makusudi na baadhi
ya wananchi bila kujali kama husababisha madhala kwa watumiaji wa maji na
kuhatarisha uhai wa viumbe hai majini”.
Shughuli
mbalimbali zinaendelea wiki hii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya
Mazingira duniani ambapo Kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika katika uwanja wa
Furahisha Mkoani Mwanza.Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
kilele cha maadhimisho hayo ambapo atashiriki katika zoezi la kuwakabidhi tuzo
washindi mbalimbali ambao wameshiriki vyema katika shughuli za utunzaji wa
mazingira.
Na:Gsengo Blog
Na:Gsengo Blog
No comments: