LIVE STREAM ADS

Header Ads

WANANCHI WA WILAYA UKEREWE MKOANI MWANZA WAILILIA CCM, WASEMA KAMA NI ADHABU IMETOSHA.


Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi Mkoa wa Mwanza kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Alfred Wambura, amebainisha kwamba CCM imejipanga vyema katika kuhakikisha inapata ushindi mnono katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa sanjari na Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.

Mjumbe huo alitoa kauli hiyo hivi karibuni Mkoani Mwanza wakati akizungumza na Radio Metro juu ya Mstakabali wa Chama cha Mapinduzi CCM, sambamba na uteuzi wake uliofanyika mwezi uliopita ambapo aliteuliwa kuwa Kamanda wa Vijana wa CCM katika Kata ya Nyakato Wilayani Ilemela.

Alibainisha kwamba hivi sasa CCM ni kama imeamka kutoka usingizini baada ya kujisahau na kujikuta inapoteza baadhi ya majimbo katika uchaguzi uliopita ambapo baadhi ya majimbo yalichukuliwa na vyama vingine vya upinzani.

“Yaani ninachokuhakikishia ni hivi CCM tumeamka, Tumeamka unajua mimi huwa natumia msemo kwamba hawa wapinzani ni kama jogoo ndani ya nyumba, mara nyingi jogoo ndani ya nyumba linapowika huwa linamuasha mwenye nyumba kwamba kumekucha…sasa wapinzani wametuamsha, na sasa hivi tumejipanga, hamtaamini kitakachotokea kuanzia serikali za mitaa mpaka serikali kuu…”Alisema Wambura.

Aidha aliongeza kuwa katika ziara zake ambazo amekuwa akifanya katika maeneo mbalimbali Mkoani Mwanza akiwa kama Mjumbe wa CCM Mkoa wa Mwanza, amekumbana na vilio kutoka kwa wananchi wakiwa wanajutia kuwachagua wapinzani wao katika maeneo yao hali ambayo inawapa imani Wafuasi wa CCM kuyarejesha maeneo hayo mikononi mwao.

“Mfano nimezunguka katika Wilaya ya Ukerewe kama mjumbe wa kamati ya utekeleza wazazi Mkoa, wale ambao walifanya makosa hayo ya kusema CCM tumechoka ngoja tujaribu upande wa pili wanalia kilio ambacho huwezi kuamini mpaka mwananchi mmoja akasema kwamba jamani CCM kama ni adhabu imetosha tunaomba basi mtusikilize na sisi, tukawaambia kutenda kosa si kosa…” Alisema Wambura huku akibainisha kwamba wanainchi hao wanalia kutokana na kukosekana kwa huduma za msingi katika Wilaya hiyo baada ya Viongozi wa upinzani waliowachagua kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Mjumbe huyo Alfred Wambura mbali ya kuwa Mjumbe wa Jumuia ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Mwanza pia ana nafasi nyingine nyingi ambazo anazisimamia ambazo ni pamoja na mwenyekiti wa mtaa wa National Magharibi sanjari, mwenyekiti wa wenyeviti wa Kata ya Nyakato wanaotokana na Chama cha Mapinduzi sanjari na kuwa Kamanda wa UVCCM Kata ya Nyakato Wilayani Ilemela.

“Kazi yangu ya kwanza kabisa kwa vijana ni amani na utulivu kwa sababu siku zote wavunja amani huwa ni vijana na hasa hawa wanaokariri wanaoambiwa tu maneno ya kukariri wanaripuka bila kuyatathmini na kuyafanyia uchunguzi…” Alisema mzee wa wambura baada ya kuchaguliwa kuwa kamanda wa UVCCM Kata ya Nyakato.

No comments:

Powered by Blogger.