LIVE STREAM ADS

Header Ads

ALICHOKIZUNGUMZA MAKAMU WA RAIS MKOANI MWANZA, KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI.



Makamu wa Rais Dkt.Mohamed Gharib Bilal amebainisha kwamba shughuli za kibinadamu zisizozingatia uhifadhi wa Mazingira zimesababisha athari za mabadiliko ya Tabianchi, na hivyo kusababisha Sekta mbalimbali za Uzalishaji hapa nchini kuathirika na athari hizo.

Dkt.Bilal ameyasema hayo hii leo Mkoani Mwanza, katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Katika Uwanja wa Furahisha Wilayani Ilemela.

Amesema kuwa nchi imeshuhudia mabadiliko ya Tabianchi katika sekta mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo sekta za Kilimo, Ufugaji, Maji pamoja na Nishati na hivyo kuhatarisha shughuli za Uzalishaji hapa nchini.

"Sekta ya kilimo imeathirika sana kutokana na ukosefu wa mvua (ukame) na hivyo kuhatarisha uzalishaji wa chakula katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Mwanza ambao mwaka huu kuna hatari ya upungufu wa chakula katika Mkoa wa Mwanza" 
Kutokana na athari hizo za mabadiliko ya Tabianchi, Dkt.Bilal amesema kuwa ni muhimu kila mwananchi kwa nafasi yake kuchukua hatua za kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabianchi ikiwa ni pamoja na kuzingatia shughuli zisizoathiri Mazingira.

Aidha amehimiza zaidi juu ya shughuli za upandaji miti ambapo ameiagiza Wizara husika kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kushirikiana kwa pamoja katika kuboresha hali ya Uhifadhi wa Mazingira hapa nchini ikiwemo kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
                                                             
Katika Maadhimisho hayo, Tuzo na Zawadi mbalimbali zimetolewa kwa washiriki ambao walishiriki katika Mashindano ya Uhifadhi wa Mazingira, ikiwemo Mashindano ya Majiji hapa nchini, ambapo kwa mara ya Tisa katika Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira, Jiji la Mwanza limeibuka kuwa Jiji la Kwanza, huku Tuzo ya Rais ya utunzaji wa Mazingira mshindi akiwa ni Leon Nombo, mkazi wa Wilaya ya Mbinga ambae amejinyakulia cheti, ngao na shilingili milioni 10.

No comments:

Powered by Blogger.