LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIGOGO 184 WATIWA MBALONI KUTOKANA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA MKOANI MWANZA. KESI 101 TAYARI ZIKO MAHAKAMANI.


Watu 184 wanashikiliwa Mkoani Mwanza kutokana na kujihusisha na Biashara ya Uingizaji, Usafirishaji na Utumiaji wa dawa za Kulevya, huku Kesi 101 zikiwa tayari ziko Mahakamani kwa ajili ya Washukiwa kusomewa mashtaka yanayowakabili kutokana na kukamatwa na dawa za kulevya.

Hayo yameelezwa hii leo na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndaro Kulwijira ambae alikuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita matumizi ya dawa za kulevya duniani ambayo katika Mkoa wa Mwanza yamefanyika katika Uwanja wa Nyamagana.

Kulwijira amesema kuwa watu hao wamekamatwa kutokana na juhudi za vyombo vya usalama Mkoani Mwanza katika kuhakikisha kuwa uingizwaji, Usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya Mkoani Mwanza unatokomezwa.

Amsema kuwa hali uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya Mkoani Mwanza inatisha kutokana na ukubwa wake, ambapo amebainisha kuwa Serikali ya Mkoa wa Mwanza imejipanga vyema kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na tatizo hilo la dawa za kulevya.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya vijana 1,500 hadi elfu mbili Jijini Mwanza wanakabiliwa na tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya huku wengine zaidi ya Elfu Kumi na Tano (15,000) wakiwa katika hatari ya kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya.

Katika kupambana na utumiaji wa dawa za kulevya, jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanashauriwa kuungana kwa pamoja ili kuhakikisha matumizi ya dawa za kulevya yanatokomezwa huku wanajamii zaidi wakiasa kuwasaidia waathirika wa dawa hizo badala ya kuwatenga.

Wakisoma Risala yao hii leo mbele ya Mgeni Rasmi Ndaro Kulwijira, vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na sasa wameacha wameiomba serikali kuongeza juhudi zake katika kuhakikisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanatokomezwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kutoa elimu juu ya kupambana na dawa hizo sanjari na kutoa fursa ya elimu ya ujasiliamali kwa vijana ili kuondokana na matumizi ya dawa hizo.

Baadhi ya Vijana waliofika katika maadhimisho hayo wameeleza kuwa hujikuta wakijiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira na hivyo kuiomba Serikali kupanua wigo wa ajira ili kuondokana na utumiaji huo huku pia wakiwatumia lawama wafanyabiashara wa dawa za Kulevya Mkoani Mwanza badala ya kuwatafutia fursa za ajira kwa ajili ya wao kuweza kupata ajira.

Wadau mbalimbali wameshiriki katika Maadhimisho hayo Mkoani Mwanza, ikiwa ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari wanaopiga vita matumizi ya dawa za kulevya nchini OJADACT pamoja na Misana Foundatio yenye Tawi lake lake Pasiansi Mwanza ambayo ni taasisi inayotoa ushauri na saha kwa watu walioathirika na dawa za kulevya.

Kitaifa maadhimisho hayo ya Siku ya Kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya yamefanyika katika Mkoa wa Mbeya ambapo Kauli mbiu mwaka huu ni "Uteja wa dawa za kulevya unazuilika na kutibika, Chukua hatua".

No comments:

Powered by Blogger.