VIJANA 158 WATIWA MBARONI JIJINI MWANZA. KATI YAO 36 WAPANDISHWA KIZIMBANI.
![]() |
Picha haihusiani na habari. |
Vijana hao
walikamatwa kufuatia vurugu zilizotokea June 11 mwaka huu baada ya Mgambo wa
Jiji la Mwanza kufika katika eneo la Msikiti wa Temple maarufu kama Msikiti wa
Wahindi na kuondoa meza na vibanda vyao vya kufanyia biashara hali
iliyosababisha vurugu kutokea masaa machache baada ya bomoa bomoa hiyo.
Vijana hao
walisababisha vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kuwasha moto katika mitaa ya
Makoroboi hali iliyohatarisha usalama wa Msikiti huo wa Wahindi ambao nusra
uchomwe moto na vijana hao kabla ya kikosi cha zimamoto kufika na kuuzima moto
huo kwa madai kuwa waumini wa msikiti huo ndio wanaosababisha wao wasiruhusiwe
kufanya biashara zao karibu na eneo hilo la msikiti.
Hali hiyo
iliilazimu jeshi la Polisi, Kikosi cha Kutuliza ghasia (FFU) Mkoani Mwanza
kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya vijana waliokuwa wamekusanyika
katika mitaa mbalimbali ya katikati ya ya jiji la Mwanza na hivyo kusababisha
shughuli zote kusimama kwa zaidi ya masaa manne katikati ya Mji.
Akizungumza
jana na Radio Metro, Kamanda wa polisi Mkoani Mwanza SACP.Valentino Mlowola
amesema kuwa jeshi la polisi litaendelea kushiriana Halmashauri ya Jiji la
Mwanza katika kuhakikisha kuwa biashara katikati ya mji zinafanyika katika
maeneo ambayo yameruhusiwa kisheria na si vinginevyo.
"Metro
Radio iko mjini Mwanza, wewe kama mwandishi wa Mjini mwanza umepita katika
maeneo ambayo zamani yalikuwa hayapitiki. Hivi sasa unaona njia zimefunguka,
mji uko safi na wale ambao walikuwa wanaleta purukushani wamedhibitiwa na
wameanza kuelewa lengo letu lilikuwa zuri kwamba tuweke mji katika hali ya
amani na usafi na wanapaswa wafuate maeneo ambayo City Council imeelekeza watu
wafanyie biashara…”. Alisema Kamanda Mlowola.
Alipoulizwa
kuhusiana na vijana waliokamatwa katika vurugu za machinga zilizotokea jijini
mwanza alisema “Siyo vijana kumi waliokamatwa ndugu yangu, waliwakamata watu 158.
Katika 158, 36 wamefikishwa mahakamani, hili ni jiji lazima liendeshwe kwa
taratibu. Ukiona unashindwa kuendesha maisha yako jijini kwa kufuata taratibu
nakushauri hapa sio mahali pako pa kukaa, nenda ziwani kavue, nenda kijijini
kasukume jembe au kashiriki katika mambo ya mifugo mifugo huko hapa town
tunataka watu ambao wanafuata taratibu…”.Alisema Kamanda Mlowola bila kuainisha
kama ambao hawajapandishwa kizimbani bado wanashikiliwa na jeshi hilo ama
wameachiwa huru.
No comments: