LIVE STREAM ADS

Header Ads

WADAU WA ELIMU WILAYA YA NYAMAGANA MKOANI MWANZA WAKERWA NA CHANGAMOTO ZA ELIMU HAPA NCHINI.

Mdau wa Elimu kutoka Taasisi ya The Desk and Chair Foundation akitoa mchango wake katika Mdahalo wa Wadau wa Elimu Jijini Mwanza uliofanyika leo katika Ukumbi JB BelMount.

Anna Sule ambae ni Katibu wa Wazazi Wilaya ya Nyamagana
Jimmy Luhende kutoka Shirika la ADLG (Kulia) akiwa na Rogers Willium Kutoka Sahara Communication (Kushoto). Katika Mdahalo huo Luhende aliwasilisha Mada ya Utawala Bora katika shule ambapo kubwa zaidi alibainisha namna utawala na usimamizi mbovu mashuleni unavyodidimiza kiwango cha elimu hapa nchini.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari hapa nchini.
Wadau wa Elimu Jijini Mwanza wameonyesha kusikitishwa kwao na Mfumo wa Elimu uliopo hapa nchini, ambapo wameuelezea Mfumo huo kuwa unawabagua wanafunzi kulingana na matabaka wanayotoka.

Wakizungumza mara baada ya uwasilishwaji wa Mada zilizotolewa katika Mdahalo wa Wadau wa Elimu Jijini Mwanza hii leo katika Ukumbi wa Hotel ya JB Belmount, wadau hao wamesema kuwa hapa nchini hakuna mfumo mzuri unaowawezesha wanafunzi kupata elimu bora kutoka na mfumo uliopo kuwagawa wanafunzi katika Matabaka ya walionacho na wasio nacho.

"Mimi naishauri Serikali ibadili sheria za elimu hapa nchini ili kila mwanafunzi aweze kupata elimu inayostahili kwa sababu kinachoendelea hivi sasa ni ukatili kwa baadhi ya mwanafunzi. Wale wanaotoka familia zenye uwezo wanafundishwa kwa mitaala na lugha tofauti na wale wanaotoka katika familia masikini nao wanafundishwa kwa lugha na mitaala tofauti, mimi nasema huu ni ukatili na Serikali haiwatendei haki wanafunzi wetu hivyo naiomba serikali hili iliangalie na kuchukua hatua ili kuwepo na lugha na mitaala ya aina moja kwa ajili ya kufundishia hapa nchini".

Katika hatua nyingine wadau hao wameelezea kusikitishwa kwao na changamoto za kielimu zisizoisha hapa nchini ambazo wamezitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa madawati mashuleni hususani kwa shule za msingi, ukosefu wa vitabu vya kufundishia, ukosefu wa vyoo bora mashuleni ambapo wameshauri kila mmoja katika jamii kuchukua hatua za kuhakikisha anakabiriana changamoto hizo na siyo kukaa na kuilaumu serikali.

"Kila kitu Serikali, Kila Kitu Serikali, je wewe unachukua hatua gani katika kukabiliana na changamoto za kielimu zilizopo hapa nchini?Wazazi hawana desturi ya kufuatilia hata maendeleo ya watoto wao, wanakaa tu kuilaumu serikali, kiukweli tunapaswa kubadilika ili kuinua kiwango chetu cha elimu hapa nchini" Walisema wadau hao.

Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI kwa kushirikiana na Wadau wengine liliweza kuandaa Mdahalo huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo Mada mbali mbali zimeweza kuwasilishwa katika mdahalo huo.Miongoni mwa mada hizo ni pamoja na Vitendo vya Ukatili na Elimu bora ambayo iliwasilishwa na Khadija Liganga kutoka KIVULINI ambapo aliainisha namna vitendo vya ukatili katika jamii vinavyodidimiza elimu kwa wanafunzi hapa nchini huku vitendo hivyo vikipelekea baadhi ya wanafunzi kukosa elimu kabisa na kuishia kutanga tanga ama hata kupoteza maisha wakati mwingine.

No comments:

Powered by Blogger.