JANUARY MAKAMBA ASHINDWA KUFICHA HISIA ZAKE. KWA KAULI HII NYUNDO LA CCM LAWEZA KUMWANGUKIA.
Licha
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwafungia kwa mwaka mmoja makada wake sita kwa
tuhuma za kuanza mapema kampeni za kugombea urais mwakani, mmoja wa makada
hao, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amekiuka maagizo ya chama chake, kwa
kutangaza kwamba ameshafanya maamuzi ya kuwania nafasi hiyo kwa asilimia 90.
Akizungumza katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London
Uingereza juzi usiku, Makamba alisema tayari ameshachukua uamuzi huo, lakini
kinachokisubiri kwa sasa ni ushauri wa mwisho kutoka kwa makundi mbalimbali
wakiwamo viongozi wa dini na wakubwa wake.
Makamba amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa Makada wa CCM wanaotaka
kuwania nafasi ya kusimamisha na CCM kupamabana na vyama vingine kuwania urais
wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwakani.
Kiongozi huyo kutoka miongoni mwa makundi ya vijana wanaotaka
kuwania urasi mwakani, hii ni mara yake ya
kwanza kutamka hadharani kuwa na nia ya kuwania urais, ingawa nyendo
zake na kauli zake siku za nyuma zilikuwa zikiashiria jambo hilo.
Nyendo hizo za Makamba na makada wengine watano waandamizi wa CCM
wanadaiwa kufanya harakati za chini kwa chini kuwania urais kabla ya wakati,
zilipelekea Februari, mwaka huu, CCM
kutoa onyo kali dhidi yao.
Makada wengine waliopewa onyo hilo na Kamati Kuu ya (CC) pamoja na
Makamba, ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye; Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Mbali na kupewa onyo kali, makada hao pia walitakiwa kutojihusisha
na kampeni au vitendo vyovyote
vinavyoashiria kampeni na watakuwa chini ya uangalizi katika kipindi cha
mwaka mmoja.
Mbunge huyo wa Bumbuli
(CCM) kwa muda mrefu amekuwa akishawishi umri wa kugombea urais upunguzwe ili
vijana nao wapate nafasi ya kuwania nafasi hiyo. Makamba, kwa sasa ana umri wa
miaka 40 kwani alizaliwa Januari 28, 1974.
Novemba mwaka jana, Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri
Kuu (NEC) ya CCM, alisema anatafakari kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa
2015 kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea
nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
NEC ya CCM ilishapiga marufuku wanachama wa chama hicho kutangaza
nia ya kuutaka urais kwa maelezaoi kuwa, kufanya hivyo ni sawa na kufanya
kampeni kabla ya wakati. Makamba, pia alizungumzia mchakato wa kutengenza Katiba Mpya,
ambao kwasasa umekwama katika Bunge la Maalum la Katiba baada ya wajumbe
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia bunge hilo.
Alisema hadi sasa mchakato huo unaonekana kushindwa kufikia
maridhiano na wanasiasa wameshindwa kuwapatia Watanzania Katiba wanayoitarajia. Hata hivyo alishauri kwamba, kama mwafaka utashindwa kupatikana
katika Bunge hilo kutokana na mivutano ya wanasiasa, mchakato huo usimamishwe
na uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa kutumia Katiba ya sasa ya mwaka 1977.
Makamba alikuwa Londoni kuhudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano
juu ya namna mpya, maarifa mapya na teknolojia mpya za kuendesha mitandao ulioandaliwa
na kampuni ya Macktech na Total Telecom ili kusaidia nchi katika sekta ya
mawasiliano.
No comments: