LIVE STREAM ADS

Header Ads

KOMBE LA MEYA JIJINI MWANZA KUANZA KWA MBWEMBWE. PEPSI YAMWAGA VIFAA UTADHANI NI LIGI KUU VILE.



Zoezi la ugawaji wa vifaa kwa timu 22  zitakazoshiriki kwenye mashindano ya Pepsi Kombe la Meya kwa mwaka huu wa 2014 limefanyika hii leo kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana jijini Mwanza.

Kila timu imekabidhiwa seti moja ya jezi na mipira miwili kwenye zoezi ambalo limesimamiwa na wadhamini wa mashindano hayo kampuni ya SBC kupitia kinywaji cha Pepsi na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Stanslaus Mabula.

Mashindano hayo ambayo kwa mwaka huu yanafanyika kwa mara ya pili yataanzaAugust 2 na kuhitimishwa Septemba 20 huku timu shiriki 22 kutoka halmashauri ya jiji la Mwanza zikiwa zimegawanywa kwenye makundi manne.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mwanza,Stanslaus Mabula amesema kuwa mashindano hayo yatumike katika kuinua vipaji vya wachezaji huku akiahidi kuwa timu zitakazofika robo fainali pia zitapewa vifaa vingine.

Mabula ametoa onyo kwa timu au mchezaji atakayeonyesha utovu wa nidhamu kwa kusema kuwa adhabu zitatolewa huku akisisitiza kamati ya mashindano hayo itakuwa makini katika kuhakikisha  wachezaji mamluki hawachezi.

Bingwa kwenye Pepsi Kombe la Meya mwaka huu atapata zawadi ya bajaji ya kisasa ya mizigo,TSH.Milioni 1.5,Kombe na medali ya dhahabu  huku kitu pekee zaidi mwaka huu ni kutumika kwa waamuzi wanafunzi wa Alliance School Sports Academy.

Mashindano haya yanafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo chini ya udhamini wa Kampuni ya SBC inayotengeneza vinywaji baridi kupitia kinywaji chake cha Pepsi ambapo kwa mwaka huu yameboresha zaidi kwa kuhakikisha vifaa vitakavyotolewa vinakuwa na ubora ikiwa pia na ongezeko la ukubwa wa zawadi za washindi. Jionee wakati timu zikipokea vifaa vya michezo hii leo katika Uwanja wa Nyamagana.

 “Lengo kubwa la mashindano haya ni kuwezesha vikundi vya vijana wajasiriamali, kuleta umoja, hamasa, kuendeleza vipaji vya soka, mshikamano na burudani, lakini pia kuviwezesha mitaji ya kuendesha shughuli zao kupitia mashindano ya soka ili kuvijengea uwezo,”
Zawadi kwa washindi mwaka huu zimeongezeka ambapo bingwa atajinyakulia Bajaji ya kisasa ya kubeba mizigo na watu wanne yenye thamani ya milioni 4.5 na fedha tasilimu milioni 1.5 (jumla milioni sita), mshindi wa pili milioni 2, mshindi wa tatu milioni 1 huku mfugaji bora, timu yenye nidhamu na mwamuzi bora kuzawadiwa Sh. Laki mbili.

Timu zitakazoshiriki michuano hiyo zimegawanywa katika makundi manne ambapo kundi A litakuwa na timu sita, kundi B, C na D kila moja litakuwa na timu tano, mzunguko wa kwanza utachezwa kwa mtindo wa ligi katika makundi na hatua ya robo fainal timu zitacheza kwa mtoano hadi kupata timu mbili zitakazo cheza fainali ili kumpata bingwa kwa mwaka 2014.

“Viwanja vitakavyotumika katika michuano ya Kombe hilo ni Nyamagana, Nyegezi Kona, Mabatine Polisi, Buhongwa, Igoma Mnadani na Mkolani na waamuzi watakaochezesha mashindano hayo ni vijana wanafunzi kutoka katika Kituo cha Michezo cha Alliance cha jijini hapa,” alieleza mratibu wa mashindano hayo upande wa kanuni Mohamed Bitegego.
 

Moja kati ya kanuni za mashindano ya Pepsi Kombe la Meya 2014, zinaeleza kuwa timu itaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 25 kwa fomu zilizotolewa, Wachezaji wa Ligi kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza hawataruhusiwa katika mashindano haya.

Ni kosa kumchezesha mchezaji ambaye hajasajiliwa. Timu itakayo mchezesha mchezaji ambaye hayupo kwenye orodha ya wachezaji waliosajiliwa itapoteza michezo yote ambayo mchezaji huyo aliichezea.

Mchezaji hatoruhusiwa kusajiliwa kwenye timu zaidi ya moja. Iwapo mchezaji huyo akibainika ataondolewa kwenye mashindano na timu hiyo haitoruhusiwa kuweka mchezaji mwingine mbadala, timu itanyang'anywa pointi kwa michezo aliyo cheza mchezaji huyo.

Mashindano yatasimamiwa na Kamati ya Mashindano ambayo inamamlaka ya kuifuta katika mashindano timu yoyote ambayo wachezaji wake watakuwa ni chanzo cha vurugu katika mashindano.
Mwanzilishi wa Mashindano ya Kombe la Meya, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza ambae pia ni diwani wa Kata ya Mkoalani (CCM).
Kila timu ina wajibu wa kutunza nidhamu ya wachezaji na washabiki wake ndani na nje ya mchezo.
Maamuzi ya refa yatakuwa ya mwisho katika mchezo.
Ni kapteni wa timu pekee ndiye anaruhusiwa kupeleka malalamiko kwa muamuzi ndani ya mchezo.
Timu itakayogomea mchezo itakuwa imepoteza mchezo husika na Kamati ya mashindano itakaa kuijadili timu hiyo kwa adhabu nyingine kama itaona inafaa.
Mchezo utaanza saa 10:30 jioni. Kila timu inatakiwa kufika uwanjani saa moja kabla ya mchezo kuanza.

Viongozi wa timu watatakiwa kusaini kwenye nakala ya kanuni itakayobaki kwa muandaaji wa mashindano ikiwa ni ishara ya kuwa wamezielewa na wataziwasilisha vyema kwenye timu zao ili kuboresha mchezo.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kampuni ya SBC Sharif Taki alisema kwamba tangu kuanza kudhamini mashindano hayo kwa sasa yamepanua wigo na kuwa na sula ya kitaifa  na tayari yamefanyika Morogoro, Mbeya, Dodoma na wanategemea Arusha kufanyika baada ya kumalizika haya ya Jiji la Mwanza huku pia wakianda ya kukutanisha timu za bingwa kwenye Majiji ya Mwanza, Tanga, Arusha, Mbeya na Dar es salaam.

Timu zote 22 zinazoshiriki Mashindano hayo leo zimepokea Vifaa kwa ajili ya Mashindano hayo.














Na: George Binagi @99.Metro FM & Mtanzania Media Blog, kwa ushirikiano na Gsengo Blog na Issack Wakuganda.

No comments:

Powered by Blogger.