LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEKTA YA MADINI INAKUA HAPA NCHINI. LAKINI INACHANGIA ASILIMIA KIDOGO KATIKA PATO LA TAIFA.

Wadau wa Sekta ya Madini wakiwa katika Picha ya Pamoja na Mgeni Rasmi (Wa Pili kulia waliokaa) Ndaro Kulwijira ambae ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika Mkutano wa Wadau wa Madini Mkoani Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo amebainisha kwamba Sekta ya Madini imeendelea kukua hapa nchini, japo bado sekta hiyo ina changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kuchangia pato kidogo katika Uchumi wa Taifa.

Hayo yamebainishwa hii leo  katika taarifa yake iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndaro Kulwijira, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Madini Mkoani Mwanza uliofanyika katika Ukumbi wa Gold Crest Hotel.


Amesema kuwa Sekta ya Madini imeendelea kukua kadri siku zinavyozidi kwenda, japo inakabiliwa na baadhi ya changamoto kama vile kuchangia kidogo katika pato la Taifa ikilinganishwa na sekta zingine.

Aidha amebainisha kuwa Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Sekta ya Madini imekuwa kwa wastani wa asilimia 10.42 hii ikiwa ni kati ya mwaka 2002 na 2012 huku ikikadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2025 Sekta ya Madini itaweza kuchangia katika pato la Taifa kwa takribani asilimia 10 ikilinganishwa na asilimia 3.3 ya hivi sasa.


Akizungumza nje ya Ukumbi wa Mkutano huo, Ndaro amebainisha kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwa hivi sasa ni mdogo licha ya sekta hiyo kuonekana kukua kutokana na ukwepaji wa ulipaji wa kodi unayotokana na biashara ya madini ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa madini nje ya nchi kwa njia za panya, ambapo ameshauri kuwa ili kuondokana na hali hiyo ni vyema wadau wote wa sekta ya madini wakatambulika na kufanya shughuli zao katika mfumo ulio rasmi.

 

Wadau mbalimbali wa Madini wakiwemo Viongozi wa Serikali, Viongozi wa TMAA (Tanzania Minerals Audit Agency), sanjari na Makampuni ya Migoni kama vile GGM, North Mara, Bulyahulu na Buzwagi wameshiriki katika Mkutano huo wa Wadau wa Madini Mkoani Mwanza.
Mhandisi Ally Samaje ambae ni Kamishna Msaidizi wa Ukaguzi wa Migodi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Madini nchini, Mhandisi Ally Samaje ambae ni Kamishna Msaidizi wa Ukaguzi wa Migodi amebainisha kwamba lengo la Mkutano huo ni kujadili utekelezaji wa utumiaji wa huduma mbalimbali zinazotakiwa katika migodi hapa chini kama sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.

Amesema sera hiyo inayaelekeza makampuni ya madini yanayopatikana hapa nchini kutumia huduma na maduduzi yote ambayo yanapatikana nchini bila kuyafuata nje ya nchi sanjari na kuwaajiri Watanzania kwa lengo la kuwezesha sekta hiyo kuchangia katika pato la Taifa bila kutegemea kodi wala mirabaha ya madini pekee.


John Henjewele ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara alikuwa Mmoja wa Washiriki wa Mkutano huo.

Katika hatua nyingine Samaje amekiri kwamba ni kweli vitendo vya utoroshaji wa madini hapa nchini upo, japo amefafanua kwamba utoroshaji huo hauyahusishi makampuni makubwa ya Madini huku akiongeza kuwa Serikali imechukua hatua ya kupambana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka wakaguzi katika maeneo yote ya upitishaji wa Madini kwenda nje ya nchi ambayo ni pamoja na viwanja vyote vikubwa vya ndege hapa nchini.

Amebainisha kuwa utoroshaji wa Madini uliopo kwa hivi sasa hapa nchini ni ule unaotokana na uuzwaji wa madini kiholela kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo ambao wanawauzia wageni madini hayo mitaani bila kufuata taratibu zilizopo.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndaro Kulwijira.
Baadhi ya Wadau walioshiriki katika Mkutano huo.


Mkutano huo wa Wadau wa Madini umelenga kujadili utekelezaji katika Sekta ya Madini katika kulinufaisha Taifa, kwa kuangalia hali ilivyo kwa hivi sasa na wapi kuna changamoto katika Sekta hiyo kukuza uchumi wa Taifa ili kupata majibu yatakayosaidia ukuaji wa sekta hiyo sambamba na ukuaji wa pato la Taifa.
 
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.