LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATUHUMIWA WA MAUAJI YA KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA WAENDELEA KUSOTA MAHABUSU.


Aliekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Liberatus Barlow.
Watuhumiwa wa Mauaji ya Aliekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Liberatus Barlow wameendelea kusota Rumande, baada ya
kesi ya mauaji inayowakabili kahirishwa mara kadhaa kutokana na uchunguzi wake kuwa bado haujakamilika.

Jumla ya Watuhumiwa saba wanakabiliwa katika kesi hiyo, Ambapo watuhumiwa hao ni Muganyizi Maicco Peter (30) Mkazi wa Nyakabungo Mkoani Mwanza, Chacha Wekena Mwita (50) Mkazi wa Gongo la Mboto Jijini Dar es salaam, Magige Mwita Marwa (48) Mkazi wa Bugarika Mkoani Mwanza.

Wengine ni Mganzi Edward (22) Mkazi wa Tandika Jijini Dar es salaam, Bhoke Marwa Mwita (42) Mkazi wa Mombasa Ukonga, Andallah Petro (32) Mkazi wa Mji Mwema Mkoani Mwanza na Abdulhaman Ismail Athman (28) Mkazi wa Mkudi Mkoani Mwanza.

Kwa Mara ya Kwanza kesi inayowakabili watuhumiwa hao ilitajwa tarehe 31.11.2012 katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza chini ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Angelo Rumisha na watuhumiwa wakarudishwa Mahabusi kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Katika vipindi tofauti tofauti watuhumiwa hao wameendelea kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayowakabili ambapo kwa mara ya 49 kesi hiyo ilitajwa alhamisi iliyopita ya tarehe 07.08.2014 ambapo kesi hiyo tena iliahirishwa hadi tarehe 14.08.2014 baada ya mwendesha mashtaka wa Serikali ambae ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Marehemu ACP. Liberatus Barlow ambae alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza aliuawa majira ya saa saba Usiku wa kuamkia tarehe 13.10.2012 na watu waliosadikiwa kuwa ni majambazi katika eneo la Kitangiri Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza wakati akitoka katika kikao cha harusi ya kifamilia.

HII ILIKUWA NI TAARIFA RASMI ILIYOTOLEWA KUFUATIA MAUAJI HAYO:
Kufuatia mauaji ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP, Liberatus Barlow, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema ametoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kama ifuatavyo:

1. Ndugu wananchi. Napenda kutumia fursa hii kuwapa taarifa kuhusu tukio la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barlow yaliyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo tarehe 13/10/2012 majira ya saa saba usiku Mkoani Mwanza.
2. Tukio hilo limetokea wakati kamanda huyo akitokea kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la Frolida hotel Mwanza mjini, akiwa na ndugu yake waliyeongozana nae kutoka kwenye kikao hicho. Wakati akimshusha huyo ndugu yake eneo la Kitangiri Minazi Mitatu, walitokea watu wanaosadikika kuwa ni majambazi, na kumvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi na kumuua papohapo.

3. Ndugu wananchi, kufuatia tukio hilo, tayari nimemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba kwenda mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na upepelezi wa tukio hilo.

4. Najua tukio hili limetushitua na kutuhuzunisha wote. Hivyo, wakati tukiendelea na taratibu zingine kuhusiana na tukio hilo, niwaombe wananchi wote kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao.
Mtanzania Media: R.I.P Kamanda wetu Barlow.

No comments:

Powered by Blogger.