LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATUNUKIWA VYETI NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA NCHINI TANZANIA.

Miongoni mwa Waliotunukiwa Vyeti wakiwa Katika Picha ya Pamoja na  Mkurugenzi wa TMA (KE) Dr.Agnes Kijazi na Mwakilishi wa Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni Samuel Muchemi (wa Pili Kulia).

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imewatunuku Vyeti Washiriki wa Warsha ya Uboreshaji wa Huduma za hali ya Hewa katika Maeneo ya Ziwa Victoria kwa Sekta ya Uvuvi, Usafirishaji na Kilimo hii leo.

TMA imewatunuku Vyeti vya Ushiriki washiriki wote walioshiriki katika warsha hiyo, ambao ni pamoja na Wavuvi, Wakulima, Wanahabari, Viongozi mbalimbali kutoka halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza na Sumatra.

Washiriki hao wametunukiwa vyeti hivyo, ikiwa ni ishara ya TMA kutambua ushiriki wao sanjari na michango mbalimbali walioitoa katika warsha hiyo, ambayo ilikuwa imelenga kuboresha upatikanaji na ufikishaji wa taarifa za hali ya Hewa kwa wananchi ili kuwawezesha kujiepusha na athari/ majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.


Katika Warsha hiyo, mbali ya kujadili namna ambavyo Mamlaka ya hali ya hewa inavyoweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa wananchi, pia Mradi wa Majaribio ulioendeshwa tangu mwaka jana Wilayani Sengerema uliweza kujadiliwa na namna ambavyo unaweza kusaidia kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wananchi.

Mradi huo ni ule wa Utoaji wa Taarifa za hali ya Hewa kwa njia ya Simu za Mkononi kwa wananchi, wakiwemo Wavuvi, wakulima na wasafirishaji wa Vyombo vya majini kwa lengo la kupata taarifa za utabiri wa hali ya hewa, jambo ambalo linaweza kusaidia kuwakinga na majanga ama athari mbalimbali katika shughuli zao.


Katika Majadiliano yao, washiriki wote walionyesha imani ya mafanikio juu ya mradi huo na hivyo kushauri juhudi zaidi kuongezw ili mradi huo kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi ambapo katika Wilaya ya Sengerema zaidi ya wananchi 350 waliweza kuandikisha namba zao kwa ajili ya kupokea taarifa za hali ya hewa kutoka TMA na kuzisambaza kwa wananchi wengine zaidi.

Baada ya Mradi huo kuonyesha mafanikio, TMA itaweza kuupeleka katika maeneo mbalimbali hapa nchini, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati zaidi.

Aidha TMA imeshauriwa kuboresha utendaji kazi wake zaidi na wadau wengine wakiwemo wanahabari, kama daraja la kufikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa wananchi, huku wananchi nao wakishauriwa kuzifuatilia kwa umakini taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuwaepusha na athari mbalimbali wawapo katika shughuli zao, mfano uvuvi nk.

Kwa Upande wake Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Dr.Agnes Kijazi, imeahidi kuboresha upatikanaji wa taarifa zake za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuboresha ushirikiano wake miongoni mwa wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari sanjari na idara za uokoaji kwa ajili ya kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinawafikia wananchi kwa wakati na hatua inachukuliwa mapema pale inapohitajika, mfano kunapotabiriwa hali ambayo inaweza kuleta majanga/ maafa/ athari kwa wananchi.

Warsha ya Uboreshaji wa Huduma za Hali ya Hewa katika Maeneo ya Ziwa Victoria kwa Sekta za Uvuvi, Usafirishaji wa Majini na Kilimo ilianza juzi Jumatatu Agost 18 katika Ukumbi wa Hotel ya Gold Crest Jijini Mwanza na imefikia tamati hii leo Agost 20 mwa huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) Dr.Agnes Kijazi akiwabidhi vyeti vya ushiriki, washiriki walioshiriki warsha hiyo.
Miongoni mwa Wanahabari walioshiriki katika Warsha hiyo kutoka Radio HHC Alive, Metro FM, RFA, Kwa Neema, na City kwa kufuata mtiririko walivyosimama.
Ukawadia Wasaa wa Misosi ikiwa ni katika Kuhitimisha Warsha hiyo ambayo ilianza Jumatatu Agost 18 na Kutamatishwa leo Agost 20 Katika Ukumbi wa Hotel ya Gold Crest Jijini Mwanza. KWENDA CHINI, TAZAMA PICHA WASHIRIKI WAKIPATA MSOSI.
Ahsante kwa Kutembelea Mtanzania Media Blog, KARIBU.
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.