LIVE STREAM ADS

Header Ads

KAULI YA MWAKYEMBE BAADA YA AJALI MKOANI MARA YAZUA HASIRA.


Kauli aliyoitoa Waziri wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe ya Kuagiza Makampuni ya Mabasi ya J4 Express na Mwanza Coach kufungiwa kujishughulisha na shughuli za Usafirishaji hadi pale
uchunguzi wa utendaji kazi wa Makampuni hayo utakapokamilika, imetafriwa tofauti na kuonekana kama ni ya kuwahadaa Watanzania.

Dk.Mwakyembe alitoa agizo la Makampuni hayo kufungiwa kufanya kazi kufuatia ajali iliyotokea juzi katika kijiji cha Sabasaba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara ambapo zaidi ya Watu 36 walipoteza Maisha papo hapo huku wengine zaidi ya 70 wakijeruhiwa vibaya. (Mpaka sasa Vifo vimeongeza na kufikia 39).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kauli hiyo ya Mwakyembe, Wakazi wa Jiji la Mwanza wameeleza kwamba wanasikitishwa na Kauli hiyo ambayo imekuja wakati ambao sio mwafaka kwa kuwa tayari watanzania wasio na hatia wamekwisha kupoteza maisha yao.

“Mimi huwa nashangazwa na hizi kauli za Serikali. Mara kwa mara Serikali imekuwa ikitoa kauli mbalimbali baada ya majanga kutokea, sasa mimi huwa najiuliza kwamba huwa Serikali iko wapi na huwa inafanya nini hadi matukio kama haya yanatokea. Ingekuwa inachukua hatua mapema kabla ya matukio haya kutokea hapo ingekuwa vyema”. Alisema mmoja wa wakazi wa jiji la Mwanza ambae hakuta kuandikwa jina lake.

Mwananchi mwingine nae aliongeza kwa kusema kuwa Kauli ya Mwakyembe haina tofauti na kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa kisiasa zaidi hapa nchini huku utekelezaji wake ukiwa si wa matumaini.

“Leo hii baada ya ajali kutokea anajitokeza Mwakyembe na kusema kwamba madereva wa Makampuni haya wachunguzwe…siju Makampuni yachunguzwe kama madereva wake wana sifa zinazostahili. Sasa mimi nasema, je hiyo itasaidia nini wakati tayari maisha ya wananchi yamekwisha potea. Mimi nasema hii kauli ni ya kutuhadaa sisi wananchi…” Alisema mama mmoja akiwa katika daladala Jijini Mwanza na kuongeza

“Huo uchunguzi wa utendaji kazi wa Makampuni haya na mengine yote yanayofanya safari zake hapa nchini ulipaswa kufanyika mapema na si katika kipindi ambacho ajali imetokea. Sasa mimi huwa najiuliza hivi hawa watendaji huwa kazi yao hasa ni kutoa matamko au ni kuhakikisha wanatutumikia sisi wananchi. Kuna watu wanaitwa Matrafiki sasa hao ndo ambao kabisaa nashindwa kuelewa wajibu wao barabarani. Kiukweli kauli ya Mwakyembe inatia hasira”.

Mabasi ya Mwanza Coach na J4 Express yaligongana uso kwa uso juzi ijumaa Septemba tano mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili yaliyokuwa katika mwendo kasi ambapo kila dereva alikuwa akiwahi kupita katika daraja ambalo mabasi hayo yasingeweza kupishana hali iliyopelekea pia basi moja kulikwangua gari jingine dogo na kusababisha kuitumbukia mtoni ambapo katika gari hiyo watu wawili kati ya watatu waliokuwemo walipoteza maisha.

“Ile sehemu ipo wazi kabisa, kule kuna kilima na huku kuna kilima na daraja lipo katikati, kwa hiyo wale madereva walikuwa ni wazembe na uzembe kama huu unasikitisha sana. Walikuwa wanaonana na hata lile gari dogo walikuwa wanaliona… hii hali inasikitisha sana,” alisema Dk. Mkwakyembe.

Aidha Mwakyembe alitahadharisa kwamba kuanzia sasa hivi kila basi litakalopata ajali ya kizembe ataaamuru vyombo husika vilifungie ili kuokoa maisha ya wananchi.  “Katika uongozi wangu madereva wazembe wajuwe kabisa kuwa sitaweza kuwavumilia, nitaamuru wafungiwe mara moja wakisababisha ajali za kizembe,” alisisitiza Waziri Mwayembe.

Majeruhi waliojeruhiwa katika ajali hiyo wamelazwa katika Hospital ya Mkoa wa Mara kwa ajili ya Matibabu zaidi ambapo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk.Samsoni Winani alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kujitolea damu na mahitaji mengine kwa ajili ya majeruhi wa ajali hiyo huku wale waliopata majeraha makubwa zaidi wakiwa tayari wamefikishwa katika Hospital ya Rufaa Bugando kwa ajili ya Matibabu zaidi.
Buldoza likifanya kazi ya kuichomoa gari ndogo aina ya Nissan Terano lenye nambari za usajili T 332 AKK lililoshukumwa na basi hilo mpaka kuingia mtoni.Gari hii ilikuwa na watu watatu,ambapo wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa.
Basi la Kampuni ya J4 EXPRESS lenye nambari za usajili T 677 CYC lililokuwa likitoka Musoma kuelekea Sirari Mkoani Mara likiwa limeharibika vibaya baada ya kugongana uso kwa uso na Basi lingine la Kampuni ya MWANZA COACH lenye nambari za usajili T 736 AWJ katika eneo la SabaSaba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara siku ya Ijumaa.

Basi la Kampuni ya Mwanza Coach lililokuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza linavyoonekana baada ya kugongana uso kwa uso na Basi la Kampuni ya J4 Express.

1 comment:

Powered by Blogger.