LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAANDAMANO YA CHADEMA YADHIBITIWA NA POLISI MKOANI MWANZA. CHADEMA WASEMA WANAJIPANGA KUVAMIA POLISI.

Gari la Polisi likiwa katika eneo la Gaden-Kemondo katikati ya Jiji la Mwanza likiwa katika hali ya kuhakikisha maandamano yaliyotangazwa tangu jana kuwa yanafanyika leo hayafanyiki. Mbali na hili kulikuwa na gari jingine maarufu kama kikojozi ambalo
ni mahususi kwa ajili ya kutawanya mikusanyiko ya watu huku likiwa na maji ya kuwasha.
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, leo limefanikiwa kuzima maandamano ya amani yaliyokuwa yametangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, yakiwa na lengo la Kupinga kuendelea kwa shughuli za Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Mjini Dodoma.

Maandamano hayo yalitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chadema Mkoani Mwanza Adrian Tizeba, lakini jeshi la polisi Mkoani Mwanza liliyazuia kutokana na shughuli za Mwenye wa Uhuru zilizokuwa zinaendelea Mkoani Mwanza sanjari na ujio wa Makamu wa Rais.

Baada ya vuta nikuvute hiyo baina ya jeshi la Polisi Mkoani na Uongozi wa Chadema Mkoa wa Mwanza, hatimae hii leo wananchi ambao wengi wao ni makada wa Chadema wakiwa na baadhi ya viongozi wao, walianza kukusanyika katika eneo la bustani iliyopo Kemondo Jijini Mwanza, ambapo jeshi la polisi lilifika na kuwatawanya tena bila kutumia mabomu ya machozi kama ilivyozoeleka huku baadhi ya wananchi sanjari na viongozi wa Chadema wakikamatwa.

Wakizungumzia Maandamano hayo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza pamoja na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, wameeleza kwamba, Chadema itaendelea na Msimamo wao wa kufanya maandamano yasiyo na kikomo huku wakilitaka jeshi la polisi kuwaachilia huru tena bila mashariti yoyote viongozi wa Chadema waliokamatwa, la sivyo wataitisha nguvu ya umma na kuvamia katika kituo cha polisi kwa ajili ya kuwatoa viongozi wao.
Oparesheni ya Jeshi la Polisi ikiendelea mapema hii leo katika maeneo ya katikati ya Jiji la Mwanza katika kuhakikisha kwamba maandamano ya Chadema yaliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza Adrian Tizeba hayafanyiki. Baadhi ya Viongozi wa Chadema Mkoa wa Mwanza wamekamatwa na Polisi akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza ambae alikamatwa tangu jana jioni baada ya kutangaza maandamano hayo.
Mbali na Mwenyekiti wa Chadema aliekamatwa na jeshi la Polisi Mkoani Mwanza jana jioni baada ya kutangaza maandamano hayo, viongozi wengine waliokamatwa hii leo kwa kosa la kujihusisha na maandamano yaliyopigwa marufuku ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema pamoja na Katibu Mwenezi wa Chadema wote kutoka Wilaya ya Nyamagana.

Wengine ni Mwenyekiti wa Vijana Chadmema Mkoa wa Mwanza, Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela na Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Bugogwa ambao wote wamekamatwa hii leo kwa kosa la kukusanyika pamoja kwa ajili ya maandamano.

Tofauti na Maandamano mengine ambayo yamewahi kutangazwa na kufanywa na Chadema, awamu hii wananchi Mkoani Mwanza wameonekana kutojihusisha kwa namna yoyote ile na uungaji mkono wa Maandamano hayo ambapo kila walipokuwa wakionekana makada wa Chadema wanajikusanya hii leo, wananchi walikuwa wanaonekana kujitenga nao hali ambayo imezua maswali mengi ambayo hayakupata majibu ikiwa ni pamoja na kwa nini wananchi hawakutaka kujihusisha moja kwa moja na maandamano yaliyokuwa yametangazwa. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu tamko la Chadema kuhusiana na Maandamano hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Valentino Mlowola alibainisha kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha linatumia nguvu zote kwa mjibu wa Kanuni na taratibu za Kisheria ili kuhakikisha kwamba maandamano hayo hayafanyiki, kwa lengo la kulinda amani ya Mkoa wa Mwanza ambayo kwa hivi sasa imetawala Mkoani Mwanza, kwa kuwa maandamano hayo yana lengo la kuvuruga amani hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Valentino Mlowola akizungumza siku ya jana na Waandishi wa Habari Ofisini kwake baada ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza kutangaza Maandamano kwa ajili ya kupinga kuendelea kwa shughuli za Bunge Maalumu la Katiba linaloelekea ukingoni Mjini Dodoma.
Msikilize hapa chini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maandamano hayo.



Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo kuhusiana na Maandamano yaliyokuwa yametangazwa na Chama hicho.
Msikilize hapa Chini Katibu wa Chadema Mkoani Mwanza akizungumzia Maandamano hayo hii leo ambapo ametoa kauli ya Chadema Mkoa wa Mwanza.

Waandishi wa Habari Mkoani Mwanza wakiwa katika Majukumu yao ya Kunasa Matukio kuhusiana na Maandamano ya Chadema 
Wasikilize baadhi ya Wananchi Mkoani Mwanza Wakizungumza juu ya Utayari wao kuhusiana na Maandamano yaliyotangazwa na Chadema Mkoani Mwanza.

Na: George Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.