LIVE STREAM ADS

Header Ads

JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA LAPIGA MARUFUKU MAANDAMANO YA CHADEMA.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Valentino Mlowola akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo ikiwa ni dakika chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Mwanza kutangaza kufanya Maandamano siku ya kesho ili kupinga shughuli za Bunge Maalumu la Katiba linaloelekea Ukingoni mjini Dodoma ikiwa ni katika kutekeleza kauli ya Mwenyekiti wa Chama hicho ya kufanya maandamano yasiyo na Kikomo nchi nzima ambayo aliitoa hivi karibuni katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika Jijini Dar es salaam.
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limepiga Marufuku ya Maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendelo Chadema yanayotarajiwa kufanyika
Kesho, yakiwa na lengo la kupinga kuendelea kwa Vikao vya Bunge Maalimu la Katiba linaloelekea Ukingoni Mjini Dodoma.

Kauli ya Jeshi hilo imetolewa hii leo na Kamanada wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Valentino Mlowola, ikiwa ni dakika chache baada ya Uongozi wa Chadema Mkoa wa Mwanza Kutangaza kufanya Maandamano hayo.

Kamanda Mlowola amesema kuwa Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yanayohusiana na Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa Bunge hilo linaendeshwa kwa mjibu wa Kanuni na Taratibu za Kisheria hivyo jeshi hilo haliwezi kuruhusu maandamano ambayo yanaweza kukwamisha shughuli za maendelo.

Mbali na hayo Kamanda Mlowola amesema kuwa kwa hivi sasa kuna shughuli za Kitaifa zinaendelea Mkoani Mwanza ambazo ni pamoja na shughuli za Mbio za Mbwenge sanjari na Ujio wa Makamu wa Rais, hivyo jeshi hilo haliwezi kutoa kibari kwa ajili ya Maandamano hayo kutokana na shughuli hizo.
Kamanda wa Polisi (M) wa Mwanza SACP.Valentino Mlowola.
Amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linatumia nguvu zote kwa mjibu wa Kanuni na taratibu za Kisheria ili kuhakikisha kwamba maandamano hayo hayafanyiki, kwa lengo la kulinda amani ya Mkoa wa Mwanza ambayo kwa hivi sasa imetawala Mkoani Mwanza, kwa kuwa maandamano hayo yana lengo la kuvuruga amani hiyo.

Aidha Kamanda Mlowola ametoa onyo kali kwa Uongozi wa Chadema kutofuata mkumbo wa kutaka kufanya jambo ambalo litahatarisha amani kwa wananchi ambao ndio wapiga kura wao, huku akiwatahadharisha Waandishi wa habari kuwa makini na maandamano hayo katika utekelezaji wa shughuli zao kwa kuwa jeshi la polisi haliwazui watu kufanya shughuli zao isipokuwa linawazuia watu kujihusisha na maandamano.
                                                 
Kufuatia kauli hiyo ya Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, wananchi nao wamekuwa na maoni tofauti ambapo baadhi yao wameonekana kutounga mkono uwepo wa Maandamano hayo kwa madai kwamba maandamano hayajengi badala yake yanaweza kuhatarisha suala la amani huku wengine wakiyaunga Mkono maandamano hayo japo kwa hoja ya kwamba wako tayari kuandamana endapo kama viongozi wa Chadema nao watakuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo.
                                                

Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Mwanza kupitia kwa Mwenyekiti wake Adrian Tizeba, hii leo kimetangaza kufanya maandamano siku ya Kesho Mkoani Mwanza kwa lengo la kupinga Bunge Maalumu la Katiba ambalo zimesalia siku chache kuhitimisha shughuli zake Mjini Dodoma, huku taarifa hiyo ikishindwa kuweka bayana maandamano hayo yataanzia wapi wala kuhitishiwa wapi hadi siku ya kesho ambapo suala hilo litawekwa wazi.
Wanahabari nao walipata fursa ya kuuliza Maswali, ambapo swali kubwa lilikuwa ni namna jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilivyojipanga katika kuwakakikishia usalama waandishi wa Habari.
Wanahabari walitaka kujua usamala wao baada ya Siku chacha zilizopita wanahabari kupigwa na polisi walipokuwa katika majukumu yao Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini Jijini Dare es Salam wakati Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe alipoitwa na polisi kuhojiwa juu ya kauli yake aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika hivi karibuni.

Hatimae Kamanda wa Polisi akasema kuwa jeshi hilo litahakikisha amani na utulivu vinazingatiwa na akasema jeshi hilo haliwazuii waandishi kutekeleza wajibu wao isipokuwa akawatahadharisha kutojihusisha na maandamano hayo. (Waandishi wasie sehemu ya Maandamano).
Wanahabari wakitoa Updates katika Mitandao ya Kijamii walipokuwa katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza wakati tamkoa la kupinga maandamano ya Chadema yaliyotangazwa kufanyika Kesho Mkoani Mwanza kupinga shughuli za Bunge Maalumu la Katiba linaloelekea Ukingoni mjini Dodoma lililokuwa likitolewa na SACP Valentino Mlowola ambae ni Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.
Waandishi wa Habari hii leo wakiwa katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Kamanda Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza.
Na: George Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.