LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YATOA TAHADHARI KWA WANANCHI MKOANI MWANZA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamalaka ya Hali ya Hewa nchini Dr. Agnes Kijazi.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuchukua tahadhari mapema, ili kukabiliana na Mvua zinazotarajiwa kunyesha katika Kipindi cha Mwezi Octoba hadi Desemba mwaka huu ili kuepukana na athari zinazoweza kusababishwa na Mvua hizo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo kwa vyombo vya habari imebainisha kwamba, mvua hizo
zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani ambapo Viwango vya uhakika kwa Mkoa wa Mwanza kupata mvua za juu ya wastani ni asilimia 45, mvua za wastani asilimia 30 na za chini ya wastani asilimia 25.

Kutokana na ongezeko hilo la wastani wa Mvua, Mamlaka hiyo imesema kuwa Mvua zinatarajiwa kuwa za kutosha kwa kilimo, malisho ya mifugo, na kuongeza chakula cha samaki katika ziwa Viktoria huku Mtiririko wa maji katika mito ukitarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya Mkoa wa Mwanza.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Vipindi vya mvua kubwa vinavyoambatana na upepo mkali vinaweza kuongeza matukio ya mafuriko, mmomonyoko wa udongo na kusabababisha vifo sanjari na uharibifu wa mali na miundombinu ya mawasiliano.

Aidha taarifa hiyo imebainisha kwamba Milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na kutuama kwa maji na utiririshaji wa maji taka usiodhibitiwa hususan maeneo ya mjini inaweza kujitokeza.

Mwelekeo wa mvua uliotolewa na Mamlaka hiyo umezingatia zaidi kipindi cha msimu cha miezi mitatu ya kuanzia mwezi Agost hadi Desemba ambapo Watumiaji wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa wameshauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini.

Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa angalizo kwamba Vipindi vifupi vya mvua kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua ambapo Mamlaka hiyo imewaondoa wasiwasi wananchi kwamba itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini kwa wananchi kadri zitakavyokuwa zikipatikana.
Na: George Binagi

No comments:

Powered by Blogger.