WASIRA ATOA ONYO KALI KWA UKAWA. ASEMA HAKUNA DAMU ITAKAYOMWAGIKA KISA BUNGE LA KATIBA.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Mkoani Mara (CCM) Steven Wasira amewakemea vikali
baadhi ya viongozi wa Kisiasa hapa nchini, wanaosema kuwa Bunge Maalumu la
Katiba lisipovunjwa amani ya nchini itavurugika.
Wasira
ametoa kauli hiyo Jijini Mwanza wakati akimsimika Kamanda wa Umoja wa Vijana wa
CCM (UVCCM) Wilaya ya Nyamagana na Kata ya Butimba Robert Masunya, katika
Mkutano wa hadhara uliofanyika jumamosi katika Kata ya Butimba.
Zaidi Wasira
aliwazungumzia Viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi UKAWA ambayo walisusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, ambao mara
kadhaa wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali zinazoashiria umwagaji damu endapo
kama Bunge Maalumu la Katiba halitasitishwa kuendelea na shughuli zake.
Amesema
wananchi wasitishwe na kauli hizo kwa kuwa amani ni haki ya watu wote kwa mjibu
wa sheria, hivyo sheria haiwezi kuwavumilia watu wachache wakaivuruga amani
iliyopo, ambapo alibainisha kuwa wanaotishia kumwaga damu ya watanzania dola
haitawavumilia kwa mjibu wa sheria.
“Wao ni
wachache, lakini kila wanachotaka wanataka kipatikane, eti kikikosekana amani
hamna…sasa leo nataka niwapashe kutoka hapa Butimba kwamba amani ni haki yetu
wote…watu wa ajabu kabisa…wao wanasema msipovunja bunge mtakiona cha mtema kuni…Mimi
nawambia hakuna cha mtema kuni na wao wakijaribu ndio watakiona cha mtema kuni...utamwaga
damu, umwage ya nani, kwa kweli kwa sheria ya Tanzania hawaruhusiwi hata
kumwaga ya kwao…kwa hiyo tunawaambia hawamwagi damu ya mtu nay a kwao
hairuhusiwi kumwagika. Dola itakuwepo kulinda damu ya yote pamoja na wao.
Habari ndiyo hiyo…”
Katika hatua
nyingine Wasira aliwataka wananchi kuwa Makini katika kuwachagua viongozi wao
ambapo alitoa pole kwa Wakazi na Wananchi wa Jimbo la Nyamagana na Ilemela kwa
makosa waliyoyafanya kwa kuwachagua viongozi wa upinzani ambao wameshindwa
kuwatumikia vyema badala yake wamekuwa wakiwachochea kufanya fujo na kushiriki
katika maandamano mbalimbali.
Wasira
alibainisha kwamba Serikali katika Mpango wake wa pili wa Maendeleo imeandaa
mikakati mbalimbali itakayowasaidia vijana katika kujikomboa na wimbi la
ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha vijana wenyewe kujiajiri katika shughuli
mbalimbali ikiwemo kilimo na uvuvi wa kisasa sanjari na uwekezaji katika
viwanda ambao utawawezesha vijana kupata ajira zaidi.
Aidha Wasira
alitoa rai kwa Vijana kutokubali vijana kutumika kisiasa ambapo alibainisha
kwamba katika kuwachagua viongozi wawe makini ili wasije wakarudia makosa kama
waliyoyafanya katika Chaguzi za mwaka 2010 ambapo waliwachagua viongozi wasio
na busara, huku akiwatolea mfano Mgunge wa Ilemela na Nyamagana ambao
wameshindwa kuwatumikia wananchi vyema huku akiongeza kuwa Mbunge kama Wenje
alichaguliwa kwa bahati mbaya iliyotokea kama ajali hivyo asithubutu kugombea
tena katika uchaguzi ujao.
Kwa upande
wake Kamanda wa UVCCM Wilaya ya Nyamagana na Kata ya Butimba Robert Masunga
baada ya kuapishwa, aliwashukuru vijana wa UVCCM Wilaya ya Nyamagana kwa imani
waliyompa ili aweze kuwatumikia ambapo aliahidi kushirikiana zaidi katika
kuwatumikia sanjari na kukiimarisha chama cha Mapinduzi zaidi.
Kabla ya
Mkutano huo wa hadhara, Wasira alizindua Mashina mawili ya Vijana wa CCM katika
Kata ya Butimba ambayo ni Shina la Pangoni Group na Shina la Vijana Bohari
ambapo katika Uzinduzi wa Mashina hayo Wasira aliwachangia vijana hao Fedha
taslimu kiasi cha Shilingi Laki Tano kila Moja kwa ajili ya kuwaongezea Mtaji
katika shughuli za ujasiriamali wanazozifanya vijana hao.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Herry James (Wa Kwanza kulia) akifuatilia tukio zima kwa Umakini wa hali ya juu. |
Wananchi wakimsikiliza kwa umakini Mh.Wasira. |
Wananchi wakimsikiliza kwa umakini Mh.Wasira. |
Hawa siku hiyo nayo walipewa kadi za CCM na kuwa Makada kamili wa Chama. |
Mh.Wasira akijumuika pamoja na wanachama wa CCM kufurahia ngoma ya Ritungu kutoka Mkoani Mara. |
Ritungu kutoka Mkoani Mara lilinoga sana. |
No comments: