TANESCO YATOA ONYO KALI KWA WAKAZI WA MKOA WA MWANZA.
Shirika
la Umeme nchini Tanesco limetoa onyo kali kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza
wanaolihujumu shirika hilo kwa kujiunganishia umeme bila ya kufuata taratibu hali inayolisababishia shirika hilo hasara kubwa.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Tanesco
Mkoani Mwanza Stella Hiza kufuatia kuwepo kwa baadhi ya watu kufanya
hujuma kwa kuiba umeme na hivyo kuwataka wenyeviti wa
mitaa kuwa makini katika swala hilo kwani wanao uwezo wa
kuwabaini watu hao.
“Katika hili viongozi wa
serikali za mtaa hawawezi kulikwepa ni wazi kuwa wanawafahamu fika, watu
wanaofanya ujanja huo lakini hawataki kuwasema jambo ambalo linaisababishia
shirika hasara” alisema Hiza
Alieleza wananchi wanatakiwa
kuwa wazelendo kwa kutoa taarifa za wizi wa umeme unaoendelea kwa baadhi
ya watu wasiokuwa waaminifu jambo litakaloleta ufanisi na kuinua
maendeleo ya nchi kwa ujumla.
“Kuna watu wanatumia njia hiyo
kujinufaisha wenyewe lakini hali hiyo tunapambana nayo kwa kufanya operesheni
mbalimbali sehemu ambazo zinakuwa sugu kwa kujiunganishia umeme usiopitia
kwenye mita na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria” alieleza
Kwa upande wake Ofisa usalama wa
Tanesco mkoani hapo Ernest Massawe, alisema suala la watanzania kutokuwa
wazalendo linachangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu huku likiruhusu mianya
hiyo ya wizi kuendelea kuwepo.
Alizitaja hasara zinaweza kujitokeza
kuwa ni pamoja na kuunguliwa nyumba jambo ambalo litaleta hasara na
kusababisha vifo visivyo tarajiwa.
“Baadhi ya wananchi hawana uzalendo
wanaweza kuwa wanafahamu watu wanaofanya hujuma hizo lakini hawaoni sababu ya
kutoa taarifa wakidhani Tanesco ndiyo inapata hasara. kumbuka hata wewe
unachangia kulipa kodi, unaweza kupata ajali za moto kwa kua kiwango cha umeme
unaounganishwa hakijapimwa kitaalamu.”alisisitiza Masawe
Mkoa wa Mwanza una wateja takribani
elfu 70 waliounganishiwa umeme, huku maeneo ya milimani yakitajwa kuwa
ndiyo yanayoongoza kwa kujiunganishia umeme wa wizi na kwa njia zisizo salama
jambo linalosababisha hasara kwa Taifa.
Na Prisca Japhes.
No comments: