LIVE STREAM ADS

Header Ads

USHAURI KWA TANROADS MKOA WA MWANZA BAADA YA KUWEKA TAA ZA KUONGOZA MAGARI KATIKA ENEO LA BUZURUGA.

Wakala wa Barabara Mkoani Mwanza TANROADS ameshauriwa kuboresha zaidi Miundo Mbinu ya Barabara katika eneo la Buzuruga Jijini Mwanza, baada ya eneo hilo kuwekwa Taa za kuongoza Magari ili
kuondokana na Msongamano ambao umeonekana kuwa kero katika eneo hilo.

Hayo yamesemwa hii leo na baadhi ya watumiaji wa barabara hiyo wakiwemo madereva na watembea kwa miguu, kufuatia matumizi ya Taa hizo kuonekana kuongeza Msongamano wa magari badala ya kusaidia kuondoa msongamano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa Dede Petro Dede akiongoza Magari katika eneo la Buzuruga baada ya kuonekana taa zilizowekwa katika eneo hilo zinasababisha foleni ndefu.

Wameeleza kwamba wazo la kuwekwa taa hizo katika eneo hilo la buzuruga ni zuri lakini kwa sasa haliwezi kuonyesha mafanikio yaliyotarajiwa, kutokana na Taa hizo kuanza kufanya kazi wakati bado hakuna miundombinu bora ya barabara katika eneo hilo.

Miongoni mwa mapungufu waliyoyataja kuwa ni kero kwao ni pamoja na ukosefu wa alaba za barabarani zinazomuonyesha dereva ni eneo gani anapaswa kusimama pindi taa zinapoashiria asimame na hivyo madereva kujikuta wakisimama katika eneo ambalo linaleta usumbufu kwa dereva alieruhusiwa na taa kupita ama kuingia barabarani.
Watembea kwa Miguu wakiteta jambo wakijianda kuvuka barabara.
Mbali na hilo pia wamesema kuwa ukosefu wa alama za barabarani umesababisha adha kubwa kwa wananchi wanaovuka barabara kwa miguu kwa kuwa hakuna eneo linaloonyesha ni wapi mtembea kwa miguu anapaswa kuvukia huku taa zilizowekwa zikiwa mahususi kwa ajili ya magari pekee na hivyo kuleta usumbufu kwa watembea kwa miguu hali ambayo inawafanya wasimame barabarani muda mrefu.
Taa za Kuongoza Magari zilizowekwa katika eneo la Buzuruga Jijini Mwanza.
Akizungumzia uwepo wa Taa za kuongoza magari katika eneo hilo la Buzuruga, Dede Petro Dede ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Kanda ya Ziwa amesema kuwa, suala la uwepo wa taa katika eneo hilo linapaswa kuangaliwa upya ikiwa ni pamoja na kuboresha kwanza miundomindu ya barabara katika eneo hilo.

Amesema uwepo wa taa hizo umesababisha foleni kubwa kinyume na matarajio yaliyokuwa yamekusudiwa hivyo ili kuondoa usumbufu huo ni vyema barabara hiyo ikapanuliwa kwanza kabla ya kuruhusu matumizi ya taa hizo, lakini pia akasisitiza kwamba TANROADS inapaswa kuweka alama kwa ajili ya wananchi wanaovuka barabara kwa miguu ili kuondoa usumbufu ambao wananchi wanaupata kwa hivi sasa.
Juhudi za kuutafuta Uongozi wa TANROADS Mkoa wa Mwanza ili kuzungumzia suala hilo ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi juu ya mipango iliyopo inayoweza kusaidia kuondokana na msongamano wa magari ambayo umeonekana kuwa kero katika eneo hilo hazikuweza kuzaa matunda.

Kwa Upande wake Kamanda Wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Mwanza Nuru Suleman amesema kuwa, ni mapema mno kwa hivi sasa kuzungumzia malalamiko yanayotolewa na watumiaji wa barabara katika eneo hilo la Buzuruga kwa kuwa ni mapema mno kuzungumzia changamoto zilizoonekana kujitokeza kwa kuwa bado TANROADS inaendelea na ukarabati wake katika barabara hiyo.
Foleni ilikuwa ndefu kweli kweli tena majira ya saa Sita adhuhuri. Ikifika jioni ni patashika.
Matumizi ya Taa za Kuongoza Magari katika eneo hilo la Buzuruga Jijini Mwanza yalianza jana kwa lengo la kuzuia msongamano wa magari, lakini hali imekuwa tofauti kutokana na taa hizo kusababisha msongamano mkubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati maaskari wa usalama barabarani walipokuwa wakiongoza magari katika eneo hilo.
Ukweli ni kwamba lengo la uwepo wa taa hizo lilikuwa zuri lakini linakwamishwa na baadhi ya mapungufu madogo madogo ambayo ni pamoja na ufinyu wa barabara hiyo ya buzuruga (Barabara ya Musoma) kulingana na wingi wa magari yanayopita katika barabara hiyo sanjari na ukosefu wa alama za barabara. Ni matumaini yangu kuwa changamoto hizo zikitafutiwa ufumbuzi hata kama si kwa asilimia zote lakini italeta unafuu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Foleni ilikuwa ndefu kweli kweli tena majira ya saa Sita adhuhuri. Ikifika jioni ni patashika.
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.