LIVE STREAM ADS

Header Ads

WASAMBAZAJI NA WAUZAJI WA MUZIKI NA FILAMU MKOANI MWANZA WAKUTANA. WASEMA WAO SI WEZI WA KAZI ZA SANAA.

Umoja wa Wauzaji na Wasambazaji wa Muziki na Filamu Mkoani Mwanza, wamekutana na Viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabiri, kwa lengo la kuondoa usumbufu wanaokumbana nao katika shughuli zao za uuzaji na usambazaji wa kazi za Wasanii.

Umoja huo umekutana
hii leo Mkoani Mwanza katika kikao cha pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikalini ambao ni pamoja na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Mkoani Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Afisa Utamaduni Wilaya ya Nyamagana pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza.
Umoja huo umekutana chini ya Uratibu wa Chama chao cha Wafanyabiashara wa Filamu na Muziki nchini kinachofahamika kwa Kimombo kama Tanzania Video Library Association (TVLA) kufuatia malalamiko waliyoyabainisha kuwa ni usumbufumbu wanaoupata katika biashara zao kwa kuhusishwa na wizi wa kazi za wasanii hapa nchini.

Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Coconut iliyoko Nyamagana Mkoani Mwanza, Richard Jorum ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Filamu na Mziki nchini (TVLA), alisema kuwa umefika wakati wa Serikali kuwatambua Wauzaji na Wasambazaji wa kazi za Sanaa kwa kuwa wanafanya shughuli iliyohalali na wanalipa kodi tofauti na ambavyo wamekuwa wakichukuliwa kuwa ni wezi wa kazi za wasanii.
“Serikali imewatizama zaidi wasanii na kuwasahau wadau wengie kama vile wasambazaji na wauzaji wa kazi za sanaa. Mara nyingi imekuwa ikikutana na wasanii peke yao na kupanga namna ya kuzuia wizi wa kazi za wasanii na kuwasahau wasambazaji na wauzaji wa kazi za wasanii hao”. Alisema Jorum na kuongeza

“Kundi la Wauzaji na Wasambazaji ni mhimu katika kazi za sanaa, lakini limesahaulika na matokeo yake linaitwa Maharamia wa kazi za Wasanii. Tunataka kuwe na mawasiliano ya karibu baina ya makundi yote na Serikali ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa utaratibu mzuri ambapo tunaamini tunaweza kuzuia wizi wa kazi za wasanii hapa nchini” Alisema Jorum huku akisisitiza kuwa wao sio wezi wa kazi za Wasanii japo wapo watu wanchache kweli wanajishughulisha na vitendo hivyo.
Katika Kikao hicho, kwa Pamoja Wauzaji na Wasambazaji hao wa Kazi za sanaa wamekubaliana kuwafichua wale wote watakaobainika kujishughulisha na wizi wa kazi za wasanii kwa kuzinakiri kazi hizo na kuziuza kinyume na sheria.

Aidha wameiomba Serikali kuwa makini na baadhi ya watu ambao wameanza kuzunguka katika Mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Dar es salaam na Mwanza, kwa madai kwamba wanawakamata wasambazaji na wauzaji wa kazi za wasanii wasio na vibali bila kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa.
Akizungumza katika Kikao hicho, Joseph Ngoseki ambae alimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, alisema kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na usawa kwa pande zote zinazohusika na biashara ya kazi za sanaa kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wadau wote wa kazi hizo wananufaika.

Nae Lutufyo Mtafya ambae ni Afisa elimu, huduma kwa walipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Mkoani Mwanza (TRA), alisisitiza zaidi juu ya uwepo wa mawasiliano ya karibu baina TRA na wadau wote wa kazi za sanaa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wadau wote wanafanya shughuli zao kuwa kufuata taratibu ili kuondoa mkanganyiko uliopo kwa wasambazaji na wauzaji wa kazi za sanaa ambao wanasema kuwa wamekuwa wakifanya shughuli zao kwa mjibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kulipia kodi katika biashara zao.
Akizungumzia Suala la Ukamataji wa wauzaji na wasambazaji wa kazi za Sanaa kwa Upande wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Maxmillian Kailangana ambae ni Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana ambae katika Kikao hicho alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo alibainisha kuwa suala hilo ndo kwanza amelisikia hivyo watu hao wakionekana katika maeneo yao ya biashara, wawaonyeshe kwanza kibali cha Ukamataji kutoka COSOTA, Polisi na kutoka kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya na ikiwa vibali hivyo havipo basi watoe taarifa mara moja katika mamlaka husika ikiwemo ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ama Polisi.

Kwa upande wake Gloria Godfrey Rutashobwa ambae ni Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Nyamagana katika Mkutano huo alibainisha kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wake kwa wadau wote wa kazi za sanaa hivyo akahimiza ushirikiano zaidi ili kuhakikisha malalamiko na changamoto zinazoibuka hivi sasa kutokana na wizi wa kazi za wasanii zinatatuliwa kwa misingi ya sheria na taratibu zilizowekwa.
Wauzaji na Wasambazaji wa Muziki na Filamu Mkoani Mwanza.
Mwenyeki wa Umoja wa Wauzaji na Wasambazaji wa Muziki na Filamu Mkoani Mwanza (Kulia) akizungumza jambo na Viongozi wenzake wa Umoja huo.
Joseph Ngoseki ambae alimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza (Kushoto) akiwa na Gloria Godfrey Rutashobwa ambae ni Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Nyamagana katika kikao hicho.
Maafisa wa TRA waliohudhuria Kikao hicho. Wa kwanza Kushoto ni Geofrey Komoro (Tabora), Katikati ni Simon Masawe (Kagera) na wa mwisho Kulia ni Lutufyo Mtafya (Mwanza). Wote ni Maafisa elimu, huduma kwa walipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mikoa yao kwenye mabano.
Joseph Ngoseki ambae alimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza.
Richard Jorum ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Filamu na Mziki nchini (TVLA).
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.