LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATENDAJI WILAYANI TARIME WANAMUANGUSHA WAZIRI MAGUFULI.

Miezi michache tu baada ya ujenzi kukamilika, mifereji imeanza kumomonyoka kutokana na ujenzi wake kuwa katika kiwango hafifu hususani kutokana na uhaba wa theluji iliyokuwa inatumika.
Kwanza kabisa
napenda kupongeza juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kwamba barabara zote kuu hapa nchini hususani zinazounganisha Wilaya moja na nyingine ama Mkoa Mmoja na Mwingine zinajengwa katika Kiwango cha Lami.

Mara kadhaa juhudi hizo zimekuwa zikichagizwa zaidi na Waziri wa Ujenzi Dk.John Pombe Magufuli ambae mara kadhaa amekuwa akisisitiza zaidi juu ya kuhakikisha kwamba barabara zote hapa nchini zinakuwa katika kiwango cha lami tena katika hali ya ubora kwa ajili ya kusaidia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji katika Taifa.

Japo kwa mwendo wa kusua sua kama wa Kinyonga, Wananchi wa Wilaya ya Tarime wakaanza kuiona neema kutokana na Ujenzi wa Barabara ambayo asilimia kubwa ya Wananchi wa Maeneo ya inje ya mji wa Tarime wanaitegemea kwa ajili ya kufikishia mazao yao ya biashara sanjari na shughuli mbalimbali katika Mji wa Tarime.

Hapa naizungumzia barabara ya Nyamwaga ambayo inaanzania katika mji wa Tarime na kupita hadi katika Mji wa Nyamongo kuelekea hadi Mugumu Wilayani Serengereti ikiwa ni barabara tegemewa sana kwa wananchi wa vijiji vingi sana Wilayani Tarime kutokana na umhimu wake wa kuwaunganisha na mji wa Tarime.

Kwa wasioijua vyema barabara hiyo ni kwamba, katika kipindi cha mvua huwa haipitiki.Na pengine adha hiyo ndiyo iliyopelekea ujenzi wa kuiwekea barabara hiyo kuanza ikiwa ni miaka kadhaa iliyopita nyuma ambapo imekuwa ikijengwa kwa awamu kuanzia katika mji wa Tarime hadi sasa ambapo imefikia eneo Kibumaye Kijiji cha Mogabiri.

Ukweli ni kwamba barabara hiyo imekuwa ikijengwa kwa awamu tofauti tofauti huku mwonekano wake wa ubora ukiwa katika hali ya kufanana katika awamu zote ambazo imekuwa ikijengwa. Lakini  kwa leo napenda nielezee ujenzi uliomalizika hivi karibuni ambao ulianzia katika eneo la Rebu Centre na kuishia katika eneo la Kibumae.

Ujenzi huo naamini ulikuwa na wasimamizi (Watendaji) lakini ninachoweza kukisema ni kwamba Watendaji hao wanamuaibisha Waziri mwenye dhamana ya ujenzi ambae ni Dk.John Pombe Magufuli ambae siku zote amekuwa akisisitiza juu ya ujenzi wa barabara tena zenye kiwango na ubora unaohitajika.

Kinyume na matarajio hayo ya Dk.Magufuli, barabara hiyo ya Nyamwaga Wilayani Tarime katika ujenzi wa kipande cha kuanzia Rebu Centre hadi Kibumaye, Mogabiri imejengwa kwa kiwango cha kawaida sana, huku hali ikiwa mbaya zaidi katika ujenzi wa Mifereji ya Maji machafu ambayo tayari imeanza kumomonyoka ikiwa ni miezi kadhaa tu tangu ujenzi wake kukamilika.

Katika kuzungumza na wananchi waliokuwa wanashuhudia ujenzi huo, wakaeleza kwamba ujenzi huo hususani wa mifereji umekuwa katika hali ya kiwango cha chini kutokana na baadhi ya watendaji wasio waadilifu ambao walipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kuingia katika biashara haramu ya kuuza mifuko ya theluji iliyokuwa imenunuliwa mahususi kwa ajili ya ujenzi.


Hakika nikapigwa na butwaa kutokana na kauli hiyo kutoka kwa baadhi ya wananchi Wilayani humo.Na moja kwa moja wazo likanijia kwamba “BAADHI YA WATENDAJI WILAYANI TARIME WANAMUANGUSHA WAZIRI MAGUFULI” hivyo wanapaswa kuona aibu kwa kuwa sehemu ya kukwamisha juhudi za Waziri Magufuli katika ujenzi wa barabara bora na zenye viwango vinavyokubalika.
TAZAMA PICHA
Na:George Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.