LIVE STREAM ADS

Header Ads

ANAOMBA MSAADA WAKO KWA AJILI YA UPASUAJI BAADA YA KUUNGUZWA NA MAMA YAKE WA KAMBO.

Binti wa miaka 23 akiwa katika hali ya majeraha baada ya kuunguzwa na Mama yake wa Kambo baada ya kumsukuma na kuangukia katika Mafuta ya Kukaangia Samaki yaliyokuwa yamechemka.
Kwanza tunapenda kuomba radhi kutokana na picha hizi kwa namna zinavyoshtua, lakini kutokana na kwamba hii ndiyo hali halisi basi hatuna budi kuonyesha hizi picha ili kwa yule ambae ataweza kuguswa kwa hali na mali basi aweze kunyoosha mkono wake kwa ajili ya kumsaidia binti huyu ili aweze kufanyiwa upasuaji baada ya kuunguzwa na mafuta ya moto na mama yake wa kambo.

Kwa jina anafahamika kama Kabunga Mussa (23) Mzaliwa wa Kijiji cha Msozi Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, ambae kwa takribani miaka Mitatu amekuwa akisumbuka kutokana na majeraha ya moto aliyoyapata baada ya Mama yake wa Kambo anaejulikana kwa jina la Anna Leganwa Kumsukuma na kuangukia kwenye kikaangio cha samaki kilichokuwa na mafuta yaliyokuwa yamechemka.Baada ya tukio hilo mama huyo alitimkia kusikojulikana na hadi sasa hajulikani aliko.

Tukio hilo lilitokea mwaka 2011 ambapo binti huyu kipindi hicho alikuwa amehitimu darasa la saba na alikuwa akijishughulisha na biashara ya kukaanga samaki, ambapo siku tukio hilo la kuunguzwa kwake linamkumba alikuwa katika majukumu yake ya kukaanga samaki na ndipo mama yake huyo wa kambo alitokea nyuma yake na kumsukumba hali iliyopelekea kuangukia katika kikaangio cha samaki kilichokuwa na mafuta yaliyochemka hali iliyopelekea binti huyu kuungua vibaya na kupata majeraha makubwa katika sehemu za uso, shingoni na katika mkono wake wa kushoto.

Akizungumza na Mtanzaniamedia Blog & Radio Metro hii leo, binti huyu ameeleza kuwa baada ya tukio hilo alifikishwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya Matibabu ambapo alipatiwa matibabu lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi mwaka huu 2014 ambapo amepata nafasi ya kufanyiwa upasuaji ambao unatarajia kufanyika Mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba.

Binti huyo amesema kuwa ili upasuaji huo uweze kufanikiwa, anatakiwa kuchangia kiasi cha pesa shilingi Laki Moja na Elfu Hamsini hii ikiwa ni baada ya kupata nafasi ya ufadhiri wa kufanyiwa upasuaji huo hivyo ndiyo maana gharama za zoezi hilo zimeonekana kuwa nafuu japo kiasi hicho bado kimekuwa mtihani mkubwa kwake kukipata baada ya kukosa msaada wowote kutoka kwa ndugu zake akiwemo baba yake mzazi Mussa Vedastus anaeishi Ukerewe.

Wakati tukio hili linatokea binti huyu alikuwa akiishi mbali na mama yake mzazi Marium Magesa, ambae walitengana na baba yake mzazi na ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza alibahatika kumuona mama yake mzazi kufuatia tukio hili lakini mama yake hakuweza kumusaidia chochote kwani baada ya kufika nyumbani na kumuona alirudi alikokuwa akiishi awali huko huko Ukerewe katika Kijiji cha Kagunguri.

Ili kumsaidia binti huyu, wasiliana nae moja kwa moja kwa nambari za simu 0755 01 08 14. Kumbuka Kutoa ni Moyo na Si Utajiri, Hivyo kidogo unachoweza kukitoa kinaweza kufanikisha Upasuaji wa binti huyu ambao unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Kabunga Mussa (23) baada ya kuunguzwa na Mama yake wa Kambo baada ya kumsukuma na kuangukia katika Mafuta ya Kukaangia Samaki yaliyokuwa yamechemka.
Na:George Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.