LIVE STREAM ADS

Header Ads

NYERERE AWATAKA WAGOMBEA URAIS KUELEZA WATAKAVYOMALIZA TATIZO LA DAWA ZA KULEVYA.

Aliyekaa  kushoto  ni  Madaraka  Nyerere, katikakati ni Mwenyekiti wa OJADACT Edwin Soko na kulia ni Cosmas  Mahoja  ambae ni rafiki wa familia  ya  hayati Baba wa Taifa  Mwl.  Nyerere, wakiwa  kwenye  mazungumzo siku ya jana na  Uongozi  wa OJADACT  kwenye  ofisi za chama  hicho  Jengo la CCM Mkoa wa Mwanza.
 “Kama Mwl.Nyerere angekuwa hai angewataka wagombea wa nafasi ya urais wanaoibuka kila kukicha kwenye uchaguzi ujao mwakani, kutaja wazi kuwa wangewezaje kumaliza tatizo  la  kukithiri kwa dawa za kulevya linalomaliza nguvu kazi ya Taifa na kuongeza utofauti wa kipato katika jamii”.

Hayo yalizungumzwa jana Jijini Mwanza na
mtoto wa Hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere wakati alipokuwa akiongea na uongozi wa chama  cha waandishi wa habari wa kupiga  vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu Tanzania (OJADACT).

Madaraka aliwafunda viongozi wa chama hicho juu ya kuwa jasili wa kuiokoa jamii inayoelemewa na mzigo wa uteja wa matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji kwa kuitaka OJADACT  kuwauliza watangaza nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao kuwa wataweza vipi kutokemeza tatizo  la  dawa za kulevya nchini.

Madaraka aliongeza kuwa suala la   mmonyoko wa maadili ndilo linaochangia katika suala zima la  jamii kujihusisha na dawa za kulevya,  hivyo nguvu za pamoja zitahitajika katika kumaliza tatizo hilo.

“Nakumbuka Mwalimu Nyerere alikuwa akihimiza suala  la maadili kuanzia ndani ya familia yake hadi kwa Taifa ili jamii iweze kujiepusha na momonyoko wa kimaadili, hivyo ni wazi tumuenzi kwa kuyarudia maadili mema ili tumalize tatizo  la dawa za kulevya”  AlisemaMadaraka.

Naye  Bwana  Cosmas Muhoja ambae ni rafiki wa karibu wa familia ya Nyerere alisema kuwa tatizo  la  dawa za kulevya linatokana na baadhi ya watu kuwa na tamaa  ya kupata mali bila kujali athari za kimaisha kwa watu wengine, jambo ambalo limekuwa likipelekea kukithiri kwa biashara ya dawa za kulevya.

Naye Mwenyekiti wa OJADACT Edwin Soko alisema kuwa kipaumbele chao kwa rais ajaye wa watanzania ni uwezo  wake  katika kupambana na tatizo  la dawa za kulevya kwani jamii imekuwa ikiangamia kila kukicha na hakuna jitihada za kutosha zinazowekwa ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo lenyewe.

Aliongeza kuwa  OJADACT  inakusudia kufanya mdahalo wa wazi kwa watangaza nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao ili waweze kujieleza ni namna gani wataweza kumaliza tatizo  la dawa za kulevya hapa nchini, na majibu yao yatakuwa moja ya vigezo vya kupimwa na wananchi kama kweli wanaweza kuwa viongozi shupavu wa kuliongoza Taifa hili.

Soko alisema kuwa Marekani iliwahi kukumbwa na kukithiri kwa tatizo la dawa za kulevya hali iliyopelekea kuwepo kwa ajenda maalumu kwa wagombea wa nafasi ya urais katika Taifa hilo na hatimaye  Richard  Nickson alifanikiwa kuja na ajenda ambayo ilisaidia kupunguza tatizo hilo nchini Marekani.
Madaraka Nyerere (kushoto) akisisitiza  juu  ya  wagombea  wa nafasi  ya  urais  katika  uchaguzi  ujao  wapimwe  kwa  kushughulikia  tatizo  la kukithiri kwa dawa za kulevya  wakati  akiongea na uongozi  wa  OJADACT  jana  jijini mwanza , mazungumzo hayo yalifanyika katika  ofisi  ya  OJADACT  Jengo la CCM  Mkoa wa Mwanza. Katikati ni Mwenyekiti  wa OJADACT  Edwin Soko na kulia  ni Cosmas  Mahoja  ambae ni rafiki wa familia  ya  hayati Baba wa Taifa  Mwl Nyerere.
Na:Edwin Soko

No comments:

Powered by Blogger.