LIVE STREAM ADS

Header Ads

MACHINGA WATAKIWA KUJIUNGA NA SHIUMATZ ILI KUNUFAIKA NA FURSA ZILIZOPO.

Wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga Jijini Mwanza wametakiwa kujiunga na Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMATZ) ili waweze kufaidika na huduma zinazopatikana katika shirika hilo.

Wito huo umetolewa
wiki iliyopita na Mwenyekiti wa umoja huo Mkoani Masanja Matondo wakati akizungumza na wanahabari Ofsini kwake  ambapo alieleza kuwa moja ya faida ya kujiunga na Shiuma, ni pamoja na  kuwa na kitambulisho kwa kila mfanyabiashara  kitakachowasaidia katika shughuli zao.

Matondo alieleza kuwa huduma nyingine zinazopatikana katika shirika hilo, ni pamoja na kuwatafutia machinga maeneo ya kudumu ya kufanyia biashara zao na kuwawezesha kupata mikopo  kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha.

“tunashirikiana na  taasisi za kifedha  kama Equity Benki, Tujitegemee Tanzania Limited na Access Benki kwa  kupitia uongozi wa wamachinga ili waweze kupata mikopo ya kukuza na uendeleza biashara zao”alisema Matondo.

Pia alieleza kuwa taasisi hizo hutoa mikopo kwa  wafanyabiashara kwa kuangalia kama mfanyabiashara ana leseni ya biashara hivyo kupitia Shiuma machinga ambao hawana leseni ya biashara wanaweza kupata mikopo kwa kupitia katika uongozi huo.

Aidha alisema kuwa  machinga  hawaruhusiwi  kufanya biashara katika maeneo yaliyo zuiliwa na kwamba  kwa kufanya hivyo ni dhahiri kuwa watakuwa wanavunja sheria  ilizowekwa na halmashauri ya Jiji la mwanza.

Hata hivyo  Matondo aliwataka Machinga Jijini Mwanza kutambua kuwa Shiuma ni chombo kinachowasimamia katika shughuli zao, hivyo  ni vyema wakapeleka kero zao mapema ili kutafutiwa utatuzi kabla hakujatokea matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusababisha vurugu katika maeneo yao ya biashara.

Na:Prisca Japhes.

No comments:

Powered by Blogger.