LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAKAZI WA MTAA WA IGOGO JIJINI MWANZA WAKUMBWA NA BOMOA BOMOA.

Mali mbalimbali za Wananchi wanaoishi Mtaa wa Igogo-Mrungushi Jijini Mwanza baada ya kutolewa nje kwa madai kuwa eneo wanapoishi wananchi hao ambao wengi wao ni wapangaji limeuzwa.
Wananchi wa Mtaa wa Igogo-Mrungushi Kata ya Igogo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza,
leo wamepatwa na taharuki baada kuondoshwa katika nyumba walizokuwa wakiishi kwa amri ya mahakama kwa madai kwamba eneo hilo limeuzwa.


Wananchi hao ambao wengi wao walikuwa ni wapangaji sanjari na wengine ambao walikuwa na shughuli zao za kibiashara katika eneo hilo, wamekutwa na kadhia hiyo majira ya saa moja za asubuhi baada ya mali zao kuondolewa katika nyumba walizokuwa wakiishi.

Habari kutoka eneo la tukio zimeelezwa kuwa eneo zilipo nyumba walizokuwa wakiishi wananchi hao kama wapangaji lilikuwa limeuzwa, lakini kutokana na wao kupata taarifa ya kuwataka kuhama waliendelea kuishi katika nyumba hizo hadi hii leo walipovurumishwa na mali zao kutolewa nje.

Kufuatia kadhia hiyo, wananchi hayo wameelezea kusikitishwa kwao kutokana na hatua ya kuwahamisha katika eneo hilo kuchukuliwa huku wao wakiwa hawana taarifa yoyote jambo ambalo wamesema kuwa limewasababishia hasara kubwa kutokana na mali zao kuharibiwa vibaya wakati wa kuhamishwa huku nyingine zikiibiwa mbaya zaidi wakiwa hawajui pa kwenda kutokana na jambo hilo kufanyika ghafla.

Wakizungumzia tukio hilo, viongozi wa Kata ya Igogo wamesema kuwa tukio hilo hata kama limetekelezwa kwa amri ya mahakama, halijazingatia haki na sheria kwa kuwa wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo hawakupewa taarifa ya kuwataka kuondoka katika nyumba hizo.

“Hata kama mmiliki wa eneo hili alipewa taarifa ya kumtaka kuondoka katika hili eneo, bado taarifa zilipaswa kutolewa kwa wapangaji ikiwa ni pamoja na kubandika taarifa hizo katika kuta za nyumba hizi ili wapangaji kuweza kuchukua hatua ya kuhama mapema”.Alisema Maicco Maungo ambae ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Igogo.

Baada ya tukio hilo la kuwaondoa wapangaji hao waliokuwa wakiishi katika nyumba zilizokuwa katika eneo lililopo katika Mtaa wa Igogo-Mrungushi Jijini Mwanza, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Henry Matata ametoa kiasi cha shilingi Laki tano kwa ajili ya kuwasaidia wapangaji waliokumbwa na kadhia ya kuondolewa katika makazi waliyokuwa wakiishi.

Juhudi za kuwatafuta wahusika wa sakata hilo akiwemo Charles Malesa ambae ni mmiliki wa eneo hilo ambalo lilikuwa na nyumba hizo hazikuweza kuzaa matunda baada ya kutoweka ghafla katika eneo hilo kufuatia bomoa bomoa katika eneo hilo sanjari na mtu anaedaiwa kununua eneo hilo pia nae hakuweza kupatikana ili kupata ukweli zaidi juu ya sakata hilo.

Imeelezwa kuwa eneo hilo liliuzwa na aliekuwa mmiliki wake ambae ni Charles Malesa lakini uuzwaji wa eneo hilo ulileta mgogoro wa muda mrefu baina yake na mnunuaji ambae mpaka sasa amefahamika kwa jina moja la Shaa, hali ambayo iliyopelekea suala hilo kutinga katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ambayo hatimae ilitoa amri ya kuwa mmiliki wake halali ni Shaa (Mnunuaji).
Wananchi ambayo mali zao zimetolewa katika nyumba walizokuwa wakiishi wakiwa katika hali ya taharuki kufuatia kuamliwa kuondoka katika nyumba hizo kwa madai kwamba eneo hilo limeuzwa na mmiliki wake.
Shughuli za kuondoa mali zilizokuwa katika eneo hilo la Igogo-Mrungushi zikiwa zinaendelea.
Shughuli za kuondoa mali zilizokuwa katika eneo hilo la Igogo-Mrungushi zikiwa zinaendelea.
Maicco Maungo (Mwenye Miwani) ambae ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Igogo akizungumzia sakata la kuondolewa wananchi katika nyumba walizokuwa wamepanga bila kupewa taarifa licha ya kuelezwa kuwa mmiliki wa nyumba hizo alipewa taarifa ya kutakiwa aondoke katika eneo hilo lakini hakuweza kuwafahamisha wapangaji wake.
Mary Raimond ambae ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa (kushoto) akizungumza kuhusiana na sakata la wananchi waliondolewa katika eneo la Igogo-Mrungushi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Henry Matata akiwa katika eneo la tukio ambapo amejionea hali ilivyokuwa na kuahidi kutoa kiasi cha shilingi Laki Tano kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na sakata la kuondolewa katika makazi yao (Wale waliokuwa wamepanga kama wakazi.Waliokuwa wanafanya biasharara hawahusiki na msaada huo kutoka kwa Mstahiki Meya).
Na:George Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.