KATIBU WA CCM MKOA WA MWANZA AHITIMISHA ZIARA YAKE WILAYANI MISUNGWI.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza akisalimiana na Wanakijiji pamoja na wanachama wa Chama hicho katika Kijiji cha Fela ulipo Mradi wa Maji Fela wakati alipofika Kijijini hapo kwa ajili ya Ukaguzi wa Mradi huo juzi jumamosi.
Na:George GB Pazzo
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa
Mwanza Miraji Mtaturu amehitimisha ziara yake ya Siku mbili katika Wilaya ya
Misungwi Mkoani Mwanza, ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi
mbalimbali ya maendeleo Wilayani humo lengo likiwa ni kujionea utekelezaji wa
Ilani ya Chama hicho tangu mwaka 2010/15.
Katika ziara
hiyo ambayo ilianza jumamosi ya Mach 28 na kuhitimishwa jumapili ya march 29
mwaka huu, Mtaturu alikagua Mradi wa Maji ulio katika Kijiji cha Fela Kata ya
Fela, Ujenzi wa Maabara katika Shule ya Sekondari Sanjo pamoja na Zahanati ya
Kijiji cha Nyang’homango Kata ya Usagara.
Akikagua
Ujenzi wa Maabara katika Shule ya Sekondari Sanjo, Mtaturu alimtaka Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kushirikiana na wananchi pamoja na wadau
wengine wa elimu ili kuhakikisha kwamba ujenzi wa maabara katika Wilaya hiyo
unafanikiwa ili wanafunzi wapate fursa ya kusoma vyema masomo ya sayansi huku
akiahidi kuchangia mifuko 30 ya simenti kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa
wa Mwanza ili kufanikisha ujenzi wa maabara katika shule hiyo ya Sanjo.
Katika
Ukaguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyang’homango aliwapongeza wanakijiji wa
Kijiji hicho kwa kufanikisha ujenzi wa Zahanati hiyo huku pia akiwahimiza Viongozi
wa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko
wa Afya ya Jamii CHF kwa lengo la kunufaika na huduma za afya kwa gharama
nafuu.
Akizungumza na
Wananchi wa Kijiji cha Fela ulipo Mradi wa Maji Fela, Mtaturu alieleza kusikitishwa
kwake baada ya Mkandarasi TEC Contructs kupitia mhandisi mshauri KOWI kuukabidhi
mradi huo kwa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na hivyo kulipwa fedha zote
kabla ya muda wa matazamio wa miezi sita kuisha ambapo Mkandarasi huyo
ameondoka na kuacha maji hayawafikii wananchi kutokana na mabomba yanayopeleka
maji kwenye tank kwa ajili ya kuwafikia wananchi kushindwa kuhimili kasi ya
maji hayo.
Akihitimisha
ziara hiyo katika Kikao cha halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Misungwi, Mtaturu
aliwataka wataalumu wa halmashauri hiyo kuondokana na fikra potofu pindi
wanapoona viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM wanatembelea miradi ya maendeleo
kwa kuwa wao ni watumishi wa Serikali inayoongozwa na chama hicho hivyo ni
lazima chama kitembelea miradi ya maendeleo kwa ajili ya kujionea utekelezaji
wa ilani yake.
Jana jioni Mtaturu aliwasili Wilayani Kwimba kwa ajili ya mwendelezo wa ziara zake katika Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza ambapo pamoja na shughuli nyingine anatarajia kuwa na mikutano miwili ya hadhara katika jimbo la uchaguzi la Kwimba pamoja na Sumve.
SOURCE:RADIO METRO FM
SOURCE:RADIO METRO FM
No comments: