UONGOZI WA KAMBI YA KULELEA WAZEE WASIOJIWEZA BUKUMBI WILAYANI MISUNGWI WATAHADHARISHWA.
Baadhi ya Wazee wasiojiweka wanaolelewa katika kambi ya Bukumbi Misungwi Mkoani Mwanza.
Na:George GB Pazzo
Uongozi katika Kambi ya kulelea Wazee
wasiojiweza iliyopo Bukumbi Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, umetakiwa
kuimarisha mahusiano mazuri na wafadhiri mbalimbali wanaojitokeza kwa ajili ya
ufadhiri kambini hapo.
Katibu wa Chama
cha Mapinduzi CCM Mkoani Mwanza Miraji Mtaturu alitoa kauli hiyo jana,
alipotembelea Kambi hiyo ikiwa ni katika ziara yake ya siku mbili iliyoanza
jana March 28 mwaka huu kwa ajili ya kutembelea Wilaya ya Misungwi kwa lengo la kujitambulisha kwa wanachama, kuzungumza na wananchi pamoja kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Ilani ya Chama hicho katika kipindi cha mwaka 2010/15.
Alisema kuwa
amepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wazee wanaoishi katika kambi hiyo,
kuwa uongozi wa Kambi umekuwa na mahusiano yasiyo mazuri na miongoni mwa
wafadhiri katika kambi hiyo ya kulelea wazee Bukumbi hali ambayo imepelekea
mmoja wa wafadhiri hao kutishia kusitisha ufadhiri wake.
Aidha Mtaturu
aliutaka Uongozi wa kambi hiyo kuwajibika katika majukumu yake kwa lengo la
kutatua changamoto ndogondogo zilizopo kambini hapo ikiwa ni pamoja na ukosefu
wa umeme kutokana na kukosekana kwa fedha za kununulia luku pamoja na matatizo
katika mfumo wa Umeme katika kambi hiyo.
Katika kutatua
tatizo la Umeme na chakula kambini hapo, Mtaturu kwa niaba ya Chama alikabidhi shilingi
Laki Tatu kwa ajili ya kununua Umeme, Mahindi gunia mbili, maharage kilo 30
pamoja na sukari kilo 50, huku
akimwagiza Afisa wa Kambi hiyo kuainisha matatizo ya mfumo wa umeme yanayopelekea
umeme kupotea kambini hapo kwa lengo la kusaidia kuyatatua.
Akizungumza kwa
niaba ya wazee waliopo nje ya kambi hiyo, Mzee Fabian Malima (55) alilalamikia
Marco Bundala ambae ni Afisa Mfawidhi wa kambi hiyo kutokana na kuwabagua
katika suala la matibabu pamoja na kutowajumuisha katika mgao wa msaada chakula
kinachotolewa na wafadhiri mbalimbali kambini hapo, huku Bi.Helena Emmanuel
ambae anaishi katika kambini hiyo akitoa shukurani zake kwa Chama cha Mapinduzi
kwa kuwajali na kuwapelekea msaada wa chakula.
Afisa Mfawidhi wa
Kambi ya kulelea Wazee wasiojiweza Bukumbi Marco Bundala alikana malalamiko
yaliyotolewa na Mzee Fabian Malima (55), kuwa amekuwa akiwabagua katika
mahitaji ya chakula na matibabu kwa kusema kuwa amekuwa akiwahudumia wazee wote
bila kuwabagua wanaoishi kambini ama nje ya kambi, huku akibainisha kuwa hivi
karibuni alipokea maelekezo kutoka kwa Viongozi wake kutowajumuiya wazee walio
nje ya kambi hiyo katika mgao wa chakula kinachotolewa na wafadhiri.
Msafara wa Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (hayuko pichani) ukiwa kambini Bukumbi Wilayani Misungwi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Kushoto) akikabidhi Mahindi gunia mbili, Maharage Kilo 30 pamoja na Sukari kilo 50 katika Kambi ya kulelea wazee wasiojiweza Bukumbi Misungwi Mkoani Mwanza alipotembelea kambini hapo jana. Katikati ni Afisa Mfawidhi wa Kambi hiyo Marco Bundara akiwa pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Misungwi Donald Magesa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Kushoto) akikabidhi Mahindi gunia mbili, Maharage Kilo 30 pamoja na Sukari kilo 50 katika Kambi ya kulelea wazee wasiojiweza Bukumbi Misungwi Mkoani Mwanza alipotembelea kambini hapo jana.
CHANZO: METRO FM
No comments: