LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAFANYABIASHARA SENGEREMA MKOANI MWANZA WAGOMA KUFUNGUA MADUKA YAO.

Miongoni mwa maduka yaliyofungwa katika Mji wa Sengerema Mkoani Mwanza jana.
Na:George Binagi-GB Pazzo
Wafanyabiashara wa Soko Kuu Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza jana wameingia katika Mgomo wa kutofungua maduka yao, kwa ajili ya kuishinikiza halmashauri ya Mji wa Sengerema kuwarudishia bidhaa zao zilizokamatwa kutokana na wao kugoma kulipa ushuru wa Kodi ya huduma.

Wakizungumza na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza ambae jana alihitimisha ziara yake ya Siku mbili Wilayani Sengerema, wafanyabiashara hao walisema kuwa suala linalowatatiza ni wao kutakiwa kulipa ushuru wa kodi ya huduma huku wakiwa hawajapewa elimu yoyote kuhusiana na ushuru huo ambao unafikia hadi shilingi elfu thelathini kwa mwezi kwa kila mfanyabiashara.

Akizungumza na Wafanyabiashara hao, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Zainabu Telaki, aliitaka halmashauri ya mji wa Sengerema kusitisha kwanza utozaji wa Ushuru huo hadi pale elimu ya kutosha juu ya ushuru huo itakapotolewa kwa wafanyabiashara hao huku pia akiagiza kuwa wafanyabiashara warudishiwe bidhaa zao zilizokamatwa baada ya kuwa wamepinga kutoa ushuru huo wa kodi ya huduma.

Mtaturu alikutana na Wafanyabiashara hao jana katika ofisi za chama cha Mapinduzi Wilayani Sengerema baada ya juzi wafanyabiashara hao kutawanyishwa na jeshi la polisi kwa kutumia mabobu ya kutoa machozi wakidhaniwa kuwa ni vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wakati wakiandamana kuelekea katika Mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi CCM uliofanyika katika Viwanja vya CCM Zeno Wilayani Sengerema ambapo alikuwa akiwahutubia wananchi.

Maandamano ya wafanyabiashara hao yalitawanyishwa na jeshi la polisi kutokana na taarifa zilizokuwa zimezagaa mjini Sengerema kwamba kulikuwa na vijana wa Chadema waliokuwa wameandaliwa kwa ajili ya kwenda kuvuruga mkutano huo.

Hata hivyo baada ya kubainika hawakuwa vijana wa Chadema, Katibu huyo aliomba radhi kwa niaba ya jeshi la polisi Wilayani Sengerema na hivyo kuomba kukutana na wafanyabiashara hao kwa ajili ya kusikiliza malalamiko yao.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Wa pili kulia) akizungumza na Viongozi wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu Wilayani Sengerema baada ya kugoma kufungua maduka jana. Wa kwanza kushoto ni Methew Lubongeja ambae ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Sengerema, akifuatiwa na Chasama Kamata ambae ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema na wa kwanzakulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Zainabu Telaki.
Mussa Lucas ambae ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko Kuu Wilayani Sengerema akiwasilisha sababu zilizowafanya wagome kufungua maduka siku ya jana katika kikao baina yao na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Sayi Kachwele ambae ni Mjumbe wa Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Sengerema akiwasilisha  jana kero yake kwa niaba ya wafanyabiashara wa Soko hilo katika kikao baina ya Viongozi wa Wafanyabiashara na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Baadhi ya Wajumbe wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu Wilayani Sengerema waliokutana jana katika ofisi za CCM Wilaya ya Sengerema na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Hayuko pichani) kwa ajili ya kuzungumzia keroa mgogoro baina yao na halmashauri ya Mji wa Sengerema.

No comments:

Powered by Blogger.