JIJI LA DAR ES SALAAM LAZIZIMA KUTOKANA NA MAFURIKO...SABABU ZATAJWA.
Na:Kennysalfes Salvatory-Dar es Salaam
Jiji
la dar es salaam ndilo jiji linalotajwa kuwa na idadi kubwa ya watu nchini. Duru za takwimu kwa mujibu ya sensa ya mwaka
2012 zinataja idadi ya watu kufikia Milioni Tano ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 kutoka sensa za miaka ya nyuma.
Hapana shaka tangu mwezi huu
wa Mei uanze
ukimuuliza mtu yeyote swali hili,"KATI YA JUA NA MVUA BORA
NINI?"...Wote watakujibu ...BORA JUA! Hii ni kutokana na mwendelezo mkubwa
wa mvua za masika zinazoendelea hapa na maeneo mengine yote ya ukanda wa pwani ikiwemo Tanga, Tanzibar Lindi na kwingineko na hivyo
kusababisha Shughuli nyingi hususani za uzalishaji,huduma za kijamii na nyinginezo nyingi kusimama.
Hii inatokana na miundombinu
ya usafirishaji ikiwemo barabara na madaraja kuwa katika hali tete ambapo maji yamefurika barabarani, madaraja yamevunjika kiasi cha
kulazimisha kikosi cha usalama barabarani kuzifunga baadhi ya barabara kwa
usalama wa raia na mali zao.
Kwa mujibu wa mamlaka
ya hali ya hewa nchini, imeelezwa kuwa sababu kubwa za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo
mbalimbali ya Ukanda wa Pwani hapa nchini ni kutokana
na KUWEPO KWA MGANDAMIZO MDOGO WA HEWA.
Katika maelezo yake Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka hiyo Dr.Agness
Kijaz, mvua hizo zinatazamiwa kuendelea kunyesha hadi mwishoni mwa mwezi huu huku ikielezwa kuwa kiwango cha mvua kinaweza kuongezeka hadi
kufikia Mm 50 kwa masaa 24 kikiwa ni kiwango cha juu zaidi na mvua kubwa katika
kiwango hicho ambapo awali mvua hiyo ilitegemewa
kunyesha tarehe 6 na 7 mwezi
huu na hivyo ndivyo
ilivyokuwa.
Dr.Kijazi alibainisha kuwa kiwango
cha mm 20 kwa saa 24 kitaendelea hadi tarehe 18
ya mwezi huu hivyo ni vyema tahadhari mbalimbali
zikaendelea kuchukuliwa ili kuondokana na madhara ambayo yameanza tayari
kujitokeza ikiwa ni pamoja na Uharibifu wa Miundominu.
Tayari Madaraja kadhaa yameripotiwa kuvunjika likiwemo
lile la Mbagala Kuu-Kibichi na mengine ya Kinondoni, Barabara kujaa maji, Vitu,
mali na biashara za wananchi kusombwa na maji, shule kusitisha masomo huku athari kubwa zaidi
ni ya vifo vya takribani watu wanane ikiwa imeripotiwa kutokea jijini Dar es
salaam.
kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na mamlaka ya utawala
mpaka asubuhi hii,jumla ya watu wanane wakiwemo
wanawake wa 3 na wanaume watano akiwemo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja wameripotiwa kufariki dunia huku duru zikidokeza kuwepo kwa madhara mengine makubwa
Jijini hapa.
Baadhi ya watalaamu wamekuwa wakieleza
kuwa Miundombinu ya Jiji la Dar es salaamu imeelemewa jambo ambalo limekuwa
likisababisha athari ya mafuriko kuwa kubwa zaidi Jijini hapa. Kwa kuwa mimi si
mtalaamu wa masuala hayo, naomba kuisihi Serikali kama hoja hiyo ina ukweli
ndani yake basi ishughulikiwe ili kunusuru madhara ya mara kwa mara ambayo
hutokana na mvua zinazonyesha katika vipindi tofauti tofauti. Lakini pia kwa
ndugu zangu wanaoishi mabondeni, nao ni vyema wakachukua hatua mapema na kuondoka
katika maeneo hayo kwa kuwa wao ndio waathirika wa kwanza wakati wa mafuriko.
No comments: