LIVE STREAM ADS

Header Ads

UONGOZI WA KATA YA MBUGANI JIJINI MWANZA WAKIRI MAPUNGUFU KATIKA ZAHANATI YAKE.

Diwani wa Kata ya Mbugani Hassan Kijuu (Kulia) akibonga na Alphonce Tonny Kapela (Kushoto) @Metro FM.
Na:George GB Pazzo
Uongozi wa Kata ya Mbugani Jijini Mwanza umekiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika Zahanati ya Kata hiyo huku ukibainisha kuwa changamoto hizo haziwezi kutatuliwa kwa sasa kutokana na ukubwa wake.

Diwani wa Kata ya hiyo Hassan Hashim Kijuu (Chadema) alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati akijibu malalamiko ya wananchi wa Kata hiyo ambao waliyatoa wakati wakizungumza katika Kampeni ya Mtaa kwa Mtaa inayoendeshwa na Radio Metro Fm.

Kijuu alisema kuwa licha ya wananchi kulalamikia za afya zinazotolewa katika Zahanati hiyo, pia inakabiriwa na ukosefu wa barabara inayoweza kupitisha gari au pikipiki kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kufika katika Zahanati hiyo kupaya matibabu.

Alikiri kuwa hakufurahishwa na Zahanati hiyo kujengwa katika eneo lenye mwinuko na hivyo kusababisha changamoto za miundombinu ambapo alibainisha kuwa zinahitajika zaidi ya shilingi Milioni Mia nane kwa ajili ya kukarabati barabara inayoelekea katika zahanati hiyo.

“Kwa kuwa nimeombwa na wananchi wa Kata ya Mbugani kutetea nafasi yangu ya Uongozi, changamoto hiyo pamoja na nyingine ambazo ambazo hazijatatuliwa zitatafutiwa ufumbuzi katika awamu ijayo ya uongozi baada ya uchaguzi”Alisema Kijuu.

Katika hatua nyingine Kijuu alizungumzia changamoto ya Mafuriko katika eneo la Mabatini ambapo alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya kuwahamisha wananchi waliojenga katika eneo hilo kwa kuwa wananchi wanapaswa kupewa maeneo mbadala kwa ajili ya makazi yao kabla ya kuhamishwa.

Aidha alikiri maisha ya wakazi wa Mtaa wa Nyerere B kuwa hatarini kutokana na hatari ya nyumba zao kuporomokewa na Jiwe lililopo katika Mtaa huo, ambapo alisema kuwa suala hilo bado linakwamishwa na Viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wazito katika kuhakikisha kuwa jiwe hilo linapasuliwa kabla halijasababisha madhara kwa wananchi.

“Mkuu wa Mkoa alithubutu kuniuliza kuwa kati ya Mawe na Watu kipi kilitangulia, akasema kama mawe ndiyo yalitangulia basi watu ndio wahame. Sasa watu wanahama kwenda wapi na wakati wanajenga Serikali ilikuwa inawaangalia tu. Tathmini iliyofanyika iligharimu kama Milioni Kumi na tano sasa hiyo nguvu ndiyo bado inasuasua”.Alisema Kijuu.


Hivi majuzi Wananchi wa Kata ya Mbugani na Mabatini walilalamikia Ukosefu wa huduma bora katika Zahanati yao ya Mbugani kutokana na uhaba wa dawa pamoja na miundombinu isiyofikika Zahanatini hapo huku wale wanaoishi katika Mtaa wa Nyerere B wakielezea hofu yao kutokana na Jiwe lililopo katika Mtaa huo ambao uko Kilimani ambalo liko hatarini kuporomokea nyumba zaidi ya 13 katika Mtaa huo.

No comments:

Powered by Blogger.