LIVE STREAM ADS

Header Ads

ZOEZI LA UANDIKISHAJI JIJINI MWANZA LAKABILIWA NA CHANGAMOTO KUBWA.

Na:Elisa Anatory
Wakazi Jijini Mwanza wameilalamikia serikali kwa  kutoa mashine chache za uandikishaji za Biometrick Voters Registration BVR pamoja na kutowatangazia wakazi hao juu ya tarehe rasmi ya zoezi la uandikishaji katika Mitaa yao.

Wakizungumza na Redio Metro Fm kwa nyakati tofauti wakazi wa  Kata za Buhongwa, Rwanima, Luchelele, Mkolani pamoja na Mkuyuni  walisema kuwa mashine hizo zimeonyesha mapungufu makubwa na hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.

“Jamani wengine sisi ni wajawazito hivyo tunavyoendelea kusukumana na hili jua mbona mimba zetu zitatoka?”. Zilisikika sauti za akina mama waliokuwa katika foleni ya kujiandikisha katika Kituo cha Shule ya Sekondari Mkolani kilichopo Kata ya Mkolani Jijini Mwanza.

Katika Kituo hicho kulizuka taflani wakati wa zoezi la uandikisha hii leo baada ya utaratibu wa kufuata mstari kuvurugika kutokana na kila mmoja kutaka kumtangulia mwenzake katika kujiandikisha hii ikiwa ni baada ya mashine iliyokuwa ikitumika katika kituo hicho kuharibika na zoezi kusimama kwa muda.

Aidha wakazi hao waliiomba Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC kuongeza vifaa vya kutosha ikiwa ni pamoja na kuweka mashine tatu kwa kila kituo ili kuraisisha zoezi hilo ambapo waliongeza kuwa hilo lisipofanyiwa kazi litasababisha watu wengi kutojisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Charles Nkonga Mwenyekiti Mtaa wa Ibanda katika Kata Mkolani Jijini Mwanza alikiri kuwepo kwa tatizo la BVR kuharibika huku akibainisha kuwa zoezi la uandikishaji katika Mtaa wake limechelewa kuanza kutokana na mashine hizo kuchelewa kufikishwa katika vituo vya Kujiandikishia.

Kama ilivyo katika Wilaya za Mkoa wa Mwanza, zoezi la Uandikishaji katika Wilaya ya Nyamagana (Jijini Mwanza) limeanza rasmi hii leo June 09, 2015 katika Kata tano ambazo ni Buhongwa, Rwanima, Luchelele, Mkolani pamoja na Mkuyuni na linatarajiwa kufikia tamati June 15, 2015 ambapo litadumu kwa muda wa siku saba na  baada ya hapo litaendelea katika Kata nyingine.
                                             Credit:Radio Metro

No comments:

Powered by Blogger.