HUU NI ZAIDI YA UNYAMA HIVYO HAUPASWI KUFUMBIWA MACHO.
Hawa ni baadhi ya wanakikundi cha Vijana Mhonze ambapo kutoka kushoto ni Katibu wa Kikundi Nelson Jackson, Masaga Budeba, Frank Laurent, Alfred Haroon pamoja na Alex Amos.
Kikundi hicho kina wanachama 20.
Na:George GB Pazzo
Kikundi cha Vijana Mhonze kilichopo
Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza kinachojishughulisha na Mradi
wa Ufugasi wa Samaki, kimeingia hasara inayokadiriwa kufikia Shilingi Milioni
tano baada ya watu wasiofahamika kusadikika kuwa wamemwaga sumu katika moja ya
bwawa la samaki la kikundi hicho na hivyo kusababisha samaki waliokuwemo kufa.
Akizungumza jumatatu
ya wiki hii kwa masikitiko makubwa huku akionyesha Samaki waliokufa, Katibu wa
Kikundi hicho Nelson Jackson alibainisha kuwa tukio la sumu kumwaga katika
bwawa hilo lilitokea usiku wa jumapili baada ya watu wasiofahamika kuvunja wigo
na kuingia yalipo mabwawa ya samaki ambapo inaaminika kuwa walimwaga sumu
ambayo ilisababisha samaki kufa.
“Huu mradi
tuliuanza mwezi Novemba mwakani na tulianza na Mabwawa mawili ambayo yote tuliweka
samaki 500 na tayari tulikuwa tumeanza uvunaji, hata jumamosi tulikuja hapa tukavuna
samaki na kuwauza kiasi cha shilingi 80,000 lakini jambo la kusikitisha jana
tulipokuja tulikutana na majanga maana tulikuta samaki wanaelea wakiwa wamekufa”.
Alisema Jackson na kubainisha kuwa hatua hiyo imekisababishia kikundi hasara
kubwa.
Aidha
alisema kuwa mradi huo umetumia gharama kubwa tangu kuanzishwa kwake ambapo
alibainisha kuwa mbali na kuwekeza nguvu kazi yao, Uradi umekuwa ukiwagharimu
shilingi 60,000 kila baada ya wiki tatu kwa ajili ya kununua chakula cha Samaki
pamoja na gharama za mafuta ambazo wamekuwa wakitumia katika mashine wakati kubadilisha
Maji mabwawani.
Jackson
alisema kuwa wakati mradi huo unaanzishwa chini ya usimamizi wa Shirika la
Maendeleo ya Jamii na kujengeana uwezo
TAHEA lililopo Nyegezi Jijini Mwanza, vijana wote wa Mhonze
walishirikishwa ambapo walijiunga takribani vijana 100 lakini vijana hao
walikuwa wakijitoa mmoja baada ya mwingine hadi kikundi kilipobaki na vijana 20
ambao waliendelea na mradi huo wa kufuga samaki.
“Wakati huu
mradi unaanza vijana wengi wa Mhonze walishirikishwa lakini leo hii
tunasikitika kuona kwamba baadhi yao wanatufanyia hivi maana tunaamini kwamba
waliomwaga sumu katika hili bwawa hawakutoka mbali, ni vijana wa hapa hapa
Mhonze ambao wamekuwa wakishinda vijiweni bila kujishughulisha hivyo napenda
kuwaambia kwamba hiki kitendo si kizuri kwani huu mradi ni wetu sote na ni bora
wangejiuka pamoja nasi na kutufanyia hivi”.Alisema Jackson.
Kwa Upande
wake Evarist Chikanga ambae ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Buganda ulipo Mradi huo alikemea
vikali tukio hilo ambapo alibainisha kuwa Serikali ya Mtaa huo ilikuwa
ikishirikiana bega kwa bega na Vijana hao tangu mradi huo uanzishwe ambapo aliwasihi
vijana kujiunga katika shughuli mbalimbali za uzalishaji badala ya kukaa
vijiweni bila shughuli yoyote na hatimae kujiingiza katika uharifu.
“Serikali ya
Mtaa wangu imekuwa ikishirikiana na vijana hawa tangu mradi huu unaanzishwa na
kwa tukio hili kitu ambacho tutakifanya ni kuhakikisha kwamba wale wote
waliohusika tunawakamatwa lakini pia tumepata funzo kubwa katika mtaa huu hivyo
suala la ulinzi shirikishi nitahakikisha kwamba linaimarishwa zaidi”. Alisema
Chikanga.
Afisa Uvuvi
Msaidizi Manispaa ya Ilemela Alpha Faustine Paragha alifika eneo la tukio na
kuchukua Sampuri ya Samaki waliokufa pamoja na Maji ya bwala linalosadikika
kuwekewa sumu kwa ajili ya kupelekwa katika maara ya Uvuvi Nyegezi Jijini
Mwanza ili kupata uhakika wa sumu iliyomwagwa bwawani huo.
“Samaki
anaweza akafa kwa kukosa hewa aina ya Oxygen lakini hapa ni karibu na Ziwa na kuna
maji mengi hivyo ni vigumu samaki kufa kwa kukosa hewa katika eneo hili na kwa
kuwa inasadikika ni sumu nitachukua sampuri ya maji na samaki waliokufa kwa
ajili ya kuipeleka katika Maabara ya Uvuvi Nyegezi ili kupata uhakika wa sumu
iliyomwagwa humu”. Alisema Paragha ambae alisikitishwa na tukio hilo.
Msimamizi wa
Vijana kutoka Shirika la Maendeleo ya Jamii na Kujengeana Uwezo Faraji Faustine
Benge alisema kuwa Mradi huo wa Samaki wa Vijana Mhonze ulianzishwa chini ya
Shirika hilo ukiwa ni miongoni mwa miradi mingine ya Vijana inayosimamiwa na
Shirika hilo katika Manispaa ya Ilemela ambayo ni pamoja na Mradi wa Ufyatuaji wa
Matofali, Ufundi Cherehani pamoja na Michezo.
“Gharama
zote ambazo zimefikiwa tangu kuanzishwa kwa mradi huu ni takribani Milioni tano
ambazo kwa sasa tunaona zimeyeyuka kwa sababu ni hasara kubwa iliyopatikana
kutokana na tukio hili, lakini sisi kama TAHEA hatuwezi kuwaacha hawa vijana
maana tutawakatisha tamaa hivyo tutashirikiana tena na Manispaa ya Ilemela ili
kuhakikisha kwamba tunaibua upya tena huu mradi maana bwawa lililoathirika ni
moja kati ya haya mawili yaliyopo hapa”. Alibainisha Benge wakati akiwa eneo la
tukio.
Ni dhahiri, shahiri kwamba tukio hili ni la kinyama na halipaswi kufumbiwa macho kwa kuwa linakwamisha juhudi za vijana kujiajiri kwa lengo la kupunguza kasi ya ukosefu wa ajira ambao umekuwa ni changamoto kubwa hapa nchini, hivyo ni vyema uchunguzi ukafanyika na wale wote waliohusika wakachukuliwa hatua za kisheria kama alivyoahidi mwenyekiti wa Mtaa wa Buganda.
Bonyeza HAPA Kutazama Picha
No comments: