KAMPUNI YA ACACIA YASHINDWA KUFANYA BIASHARA NA WAFANYABIASHARA WA MKOANI SHINYANGA.
Na:Shaban Njia
Imeelezwa kuwa Mgodi wa dhahabu wa
Buzwagi kupitia kampuni yake ya ACACIA Mkoani Shinyanga unashindwa kufanya
biashara na wafanyabiashara wa Mkoa huo kutokana na biashara zao kutokuwa na
vithibitisho pamoja na ubora mzuri hali ambayo inapelekea Mgodi huo kuagiza
mahitaji yake nje ya nchi.
Hayo yalibainishwa juzi na Meneja wa
Mgodi huo Philibert Lweimamu wakati akizungumza na
wafanyabiashara wilayani kahama ambapo alisema kuwa wafanyabiashara
Wilayani humo wanakosa fursa zitolewazo na mgodi huo kutokana na biashara zao
nyingi ikiwemo vifaa vya mgodini kutokuwa na ubora unaohitajika.
“Tunapenda kufanyabiashara na wafanyabiashara wa Kahama na maeneo jirani hii ikiwa ni njia moja wapo ya kuongeza kipato ndani ya Wilaya hii na hivyo kuleta mabadiliko, lakini jambo ambalo linapelekea sisi kutokufanya nao biashara vifaa vyao kutokuwa na grantii za uhakika hali inayotulazimu tununue vifaa kutoka nje ya nchi ama nje ya Mji wa kahama wakati fursa hizi ni za watu wa Kahama”. Alisema Lweimamu.
Kwa upande wake mtalaamu wa ugavi na Maendeleo ya masuala ya biashara ndani ya mgodi huo wa Buzwagi Nikison Mlumba alisema kuwa wafanyabiashara Wengi Wilayani Kahama wamekuwa hawana ushirikiano mzuri na Mgoni huo na kwamba biashara nyingi ndani ya Wilaya hiyo zinaendeshwa kiholela bila kufuata sheria na taratibu za kibiashara.
“Wafanyabiashara wengi ndani ya kahama wamekuwa wanafanya biashara bila kufuata sheria za biashara jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu wakati kutoa mapato na sisi kama kampuni tunashindwa kufanya biashara nao kwa kuepuka usumbufu huo”. Alisema Nikisoni.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephina Matilo alisema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuzichangamkia fursa ambazo zinatolewa na mgodi huo wa Buzwagi ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto zilizopo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassor Rufunga alisema kuwa mgodi wa Buzwagi kupitia kampuni yake ya ACACIA umekuwa ukishiriki vyema katika masuala ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na jamii, ambapo mgodi huo umejenga vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali Wilayani humo, kukarabati barabara pamoja na kujenga kituo cha afya kilichogharimu zaidi ya shilingi Milioni 600 katika Wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo Wilayni humo wameshindwa kuchangamkia fursa zinazolewa na Mgodi huo ambapo kila mfanyabiashara anataka kujinufaisha mwenye hali inayopelekea kushindwa kumudu biashara kutokana na mahitaji makubwa yanayotakiwa mgodini hapo na kubainisha kuwa kama wangeshirikiana kwa pamoja fursa hizo zisingekuwa zionapelekwa nje ya nchi.
Katika hatua nyingine amewataka wafanyabiashara Mkoani Shinyanga kushirikiana kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazotolewa na kampuni ya ACACIA na hatimae kuwa chachu ya maendeleo ya haraka katika biashara zao na Mkoa kwa ujumla.