LEMBELI NA BULAYA WAPOKELEWA VYEMA JIJINI MWANZA. CHADEMA WASEMA MGOMBEA URAIS ATATOKA UKAWA.
Mamia ya Wananchi wakiwa katika Mkutano wa Chadema uliofanyika jana Jijini Mwanza.
Na:George GB Pazzo
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema
kimesema kuwa mazungumzo miongoni mwa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi UKAWA bado yanaendelea, lengo likiwa ni kufikia maridhiano ya pamoja
na hatimae kumsimamisha Mgombea mmoja wa nafasi ya Urais kupitia Umoja huo
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman
Mbowe alitoa kauli hiyo jana Katika Uwanja wa Magomeni Kirumba Jijini Mwanza, wakati akihutubia mamia ya
wananchi katika Mkutano wa hadhara wa kuwapokea aliekuwa Mbunge wa Kahama James
Lembeli pamoja na Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Mara Ester Bulaya wote kutoka
Chama cha Mapinduzi CCM ambao wamejiunga na Chadema.
Mbowe alisema kuwa viongozi wa vyama
vinavyounda Umoja huo wanafanya juhudi zote ili kuhakikisha kwamba maridhiano
yanapatikana miongoni mwao na hatimae kufanikisha kumsimamisha mgombea mmoja wa
Urais kwa niaba ya vyama vyote hivyo wananchi wawe na subira wakati mazungumzo
yanaendelea.
“Naomba wananchi muwe na Utulivu maana
Umoja wetu wa Ukawa ni wa Msingi sana hivyo tusiwe na haraka wala tusiwe na
mihemuko. Tutambue kwamba kuna changamoto zinapatikana lakini sisi kama
viongozi tunawahakikishia kwamba tutatumia kila mbinu na kila goti litapigwa kuhakikisha
kuwa Ukawa tunamaliza salama majadiliano yetu na tunakuwa na mgombea mmoja kwa niaba ya vyama
vyote baada ya kuridhiana”. Alismema Mbowe huku akishangiliwa na umati wa
Wananchi waliokuwa katika Mkutano huo.
Hata hivyo mkutano huo ulifanyika huku
Viongozi wa Vyama vingine vinavyounda Umoja huo wa Ukawa ambavyo ni Chama cha
Wananchi CUF, NCCR Mageuzi pamoja na NLD wakishindwa kuhudhuria licha ya kupewa
mwaliko, ambapo Mbowe alisema kuwa hali hiyo ilisababishwa na mwingiliano
shughuli za kichama ndani ya vyama hivyo.
“Leo asubuhi ilikuwa nije na Mzee
Makaidi (Emmanuel Makaidi Mwenyekiti wa NLD) lakini kwa bahati mbaya kutokana
na foleni za Dar es salaam akachelewa ndege, niliongea na Mh.Lipumba (Profesa
Ibrahim Lipumba Mwenyekiti wa CUF) na Mbatia (James Mbatia Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi) lakini nao walikuwa na vikao vya ndani ya vyama vyao kwa ajili ya maandalizi
ya uchaguzi hivyo wakashindwa kufika”. Alitanabaisha Mbowe huku akiwahimiza
watanzania kuwa wavumilivu juu ya kiu yao kutaka kumjua Mgombea Urais atakae uwakilisha
Ukawa kwa kusema kuwa mgombea huyo atatangazwa muda mwafaka utakapofika.
Kwa pamoja Ester Bulaya ambae alikuwa
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) akiwakilisha Vijana Mkoani Mara na James Lembeli
ambae alikuwa Mbunge wa Kahama (CCM) baada ya kupokea kadi ya Chadema walisema
kuwa wakati umefika wa Watanzania kufanya mabadiliko kwa kuhakikisha kuwa wanaiondoa
CCM Madarakani kwa kuwa imeshindwa kutumia rasrimali zilizopo nchini kuwaletea
maendeleo.
“Nikamtoeee nisimtoeeeee…Kamtoeeee…Naniiiii…Wasiraaaaa…Wapiii…Bundaaaaaa…linii
tarehe Octoba 25…Kama anasikia atafuata ushauri wa Makongoro Nyerere kwamba
awamu ya Kwanza yupo, ya pili yupo, ya tatu yupo, ya nne yupo, lakini awamu ya
tano bye bye”. Alisema Bulaya ikiwa ni tahadhari kwa Mbunge Jimbo la Bunda Mkoani
Mara (CCM) Mh.Steven Wasira ambae pia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Hali ilivyokuwa Katikati ya Jiji la Mwanza jana baada ya Mkutano wa Chadema Kumalizika ambapo wanachadema walisindika msafara wa viongozi wa Chama hicho hadi hotelini.