LIVE STREAM ADS

Header Ads

KAULI YA MWENYEKITI WA UVCCM WILAYA YA NYAMAGANA YAIBUA MGAWANYIKO NDANI YA JUMUIYA.

Mwenyekiti UVCCM Nyamagana Mkoani Mwanza Hussein Kim
Na:Oscar Mihayo
Jumuia ya Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, imemtaka Mwenyekiti wao Hussein Kim kufuta kauli aliyoitoa juzi kwenye vyombo vya habari ya kuwa Mgombea Urais Edward Lowasa anatumia umoja wao kwenda Dodoma kuvuruga vikao vya chama hicho vya kumteua Mgombea Urais.

Akizungumza jana katika kikao cha jumuiya hiyo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kikao hicho Gharib Ahmada alisema kuwa kauli ya mwenyekiti wao aliyoitoa katika vyombo vya habari si sahihi kwa kuwa hawakukaa kama jumuiya ili kutoa kauli hiyo hivyo tamko alilotoa ni la kwake binafsi.

“Sisi kama jumuiya hatujakaa kikao zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa,tunashangaa kauli aliyoitoa Mwenyekiti wetu kwa kutumia jumuiya yetu kwani sisi tunafuata kanuni na taratibu za chama kwa yeyote atakaypitishwa tutamuunga mkono”. Alisema Ahmada.

Pia Jumuiya hiyo ilimtaka Kim kukanusha kauli yake na kama akishindwa kufanya hivyo itachukua maamuzi magumu ikiwemo kufunga ofisi na kumtaka ajiuzulu wadhifa huo kabla ya kufikishwa katika ngazi ya juu ya Chama.

Ahmada alisema kuwa mwenyekiti wao amekuwa akifanya mambo ambayo yanakiuka kanuni na taratibu za jumuiya hiyo kwani tangu 2012 hajawahi kuitisha kikao cha umoja wao kwa lengo la kujadili mwenendo wa chama Wilayani Nyamagana jambo ambalo alisema linatia shaka juu ya uongozi wake.

Akizungumza na Mwandishi wetu kwa njia ya simu, Kim alisema kuwa hawezi kutengua kauli yake kwani anayepaswa kumshauri atengue kauli aliyoitoa ni Katibu wake na si wajumbe jumuiya hiyo kama walivyo fanya.

No comments:

Powered by Blogger.