LIVE STREAM ADS

Header Ads

MVURUGANO WATOKOTA BAADA YA TANO BORA YA WANAOWANIA NAFASI YA KUGOMBEA URAIS CCM KUTANGAZWA.

Dk. Emmanuel Nchimbi akitoa malalamiko yake mbele ya vyombo vya habari mara baada ya kutoka kwenye kikao cha CC. Kulia kwake ni Adam Kimbisa.
Imeandaliwa na Mwanahalisionline
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imetoa orodha ya wagombea watano bila ya jina la mtangaza nia aliepewa kipaumbele na Watanzania Edward Lowassa kuwemo. 

Lakini katika hali inayoonesha mpasuko, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu wamepinga uamuzi huo.

Walioingia tano bora ni Bernad Membe ambae ni mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk.John Pombe Magufuli ambae ni mbunge wa Chato na Waziri wa Ujenzi, Dk.Asha Rose Migiro ambae ni mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria.

Wengine ni January Makamba ambae ni mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na Balozi Amina Ali ambae ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Marekani.

Maamuzi hayo yameonekana kutowaridhisha walio wengi wakiwemo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu hususani wanaojulikana kuwa ni waungaji mkono wa Mh.Lowassa, ambapo wamejitokeza hadharani kuyapinga huku wakilalamika kuwa kanuni zimevunjwa.


Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa walifika mbele ya vyombo vya habari mara tu kamati kuu ilipomaliza kikao chake usiku wa kuamkia leo, na kusema hawakubaliani na maamuzi yaliyotolewa.

Wajumbe hao wakizungumza kwa kupokezana huku wakitoa kauli kali, walisema kanuni za utendaji katika vikao vilivyotangulia Kamati Kuu zimekiukwa. Kamati Kuu ina wajumbe 32.

Wamesema ukiukaji umekuja pale Kamati Kuu ilipopatiwa majina matano, badala ya kupokea majina yote ya wanachama walioomba kuteuliwa, ili yenyewe ndiyo itoke na majina matano baada ya kuyafanyia uchambuzi.

“Kanuni zinasema Kamati Kuu itapokea majina ya waombaji wote na ikishafanya uchambuzi wa kila muombaji, yakiwemo maoni ya kamati ya usalama na maadili, ndiyo huchagua majina matano yanayofikishwa mbele ya Halmashauri Kuu,” alisema Dk. Nchimbi ambaye alitokea kama kiongozi wa hao wajumbe watatu.

Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, alisema hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu kwa sababu hawakutarajia Kamati Kuu itakiukwa na kupokea majina ya baadhi tu ya waombaji.

“Haijawahi kutokea tangu nilipoingia katika Kamati Kuu kushuhudia ukiukaji wa kanuni kama ilivyotokea leo (jana) hii. Tumejitahidi kuuliza kwa mwenyekiti imekuaje kanuni inakiukwa lakini tumekosa maelezo ya kuridhisha.” Alisema Simba, waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.


Hii leo NEC yenye wajumbe wapatao 378 huwa inajadili majina hayo na kupiga kura ili kuchagua majina matatu ambayo yatapelekwa mbele ya Mkutano Mkuu kwa uamuzi wa kupata mgombea.


Mgombea wa CCM anatarajiwa kutangazwa mara tu mkutano mkuu ambao utaanza mchana, utakapomaliza kupiga kura. Mkutano Mkuu una wajumbe zaidi ya 2,000.

Kabla ya hapo, itakuwa yametolewa matokeo ya kura alizopigiwa Dk. Ali Mohamed Shein aliyepitishwa kugombea tena nafasi ya urais wa Zanzibar.

No comments:

Powered by Blogger.