LIVE STREAM ADS

Header Ads

LOWASA AJIUNGA RASMI NA CHADEMA. ASEMA MAAMUZI YA CHUKI DHIDI YAKE YAMEMUONDOA CCM.

Na:George GB Pazzo
Waziri Mkuu Mstaafu na aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli Mkoani Arusha Mh.Edward Ngoyai Lowasa kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.

Mh.Lowasa ametangaza kujiunga na Chadema hii leo Jijini Dar es salaam, katika Mkutano wa wake ambao pia umehudhuriwa na viongozi wa vyama vyote vinaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mh.Lowasa amesema kuwa amefikia maamuzi ya kujiunga na chama hicho kufuatia maamuzi ya chuki na yasiyo ya haki katika mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM yaliyopelekea jina lake kuondolewa katika mchakato huo. Katika Mchakato huo CCM ilimchagua Drk.John Pombe Magufuli kuipeperusha bendera yake katika kinyang'anyiro cha Urais.

"Baada ya Kutafakari kwa kina, kuanzia leo nimetoka ndani ya CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chadema na hivyo kuungana nao kwa ajili ya kuhakikisha tunaing'oa CCM madarakani". Amesema Mh.Lowasa.

Katika hotuba yake, Mh.Lowasa amerudia kauli aliyowahi kuitoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kwamba CCM si baba wala mama yake hivyo mabadiliko yanaweza kupatikana hata nje ya CCM.

Aidha kwa mara nyingine Mh.Lowasa amekanusha kuhusika na Sakata la Ufisadi la Richmond ambapo amesema kuwa alichukua maamuzi ya kujiuzulu ili kuwajibika kwa niaba ya Serikali.

"Mtu ambae ana ushahidi wowote kuhusu Richmond aende Mahakamani na kama hakuna ushahidi Shut up and Keep quite (Nyamaza Kimya) kwani nilijiuzulu ili kuwajibika kwa niaba ya serikali, na sioni hapo kosa langu ni lipi, kwanza nilistahili kupewa tuzo". Amesema Mh.Lowasa na kuongeza;

"Niliitisha Kikao na makatibu wakuu wote na nilitaka kuvunja mkataba wa Richmond lakini Katibu Mkuu alitoka nje ya kikao kwa muda wa saa moja na aliporudi akasema kaambiwa na mamlaka za juu kuwa mkataba usivunjwe". Ametanabaisha Mh.Lowasa.

Viongozi wote wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa ambavyo ni CUF, CHADEMA, NCCR MAGEUZI na NLD wamemkaribisha Mh.Lowasa kwa mikono yote miwili huku wakimtakia kila la kheri katika safari yake ya kisiasa nchini.

"Hatukumkaribisha Lowasa peke yake, bali tumemkaribisha na mamilioni ya watu. Mimi mniletee mamilioni ya watu niwakatae, nina wazimu mimi?, Kwanza mtanifukuza kesho tu". Amesema Mwenyekiti wa Chadema Mh.Freeman Mbowe wakati akizungumza katika mkutano.

Mh.Lowasa amejiunga na Chadema siku moja tu baada ya kukaribishwa kujiunga na chama hicho ambapo wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Lowasa kusimamishwa na Ukawa ili kuipeperusha bendera yake katika kinyang'anyiro cha urais, mkakati ambao unahatarisha uhai wa CCM madarakani.

No comments:

Powered by Blogger.