LIVE STREAM ADS

Header Ads

ONGEZEKO LA WAHAMIAJI HARAMU LAMTESA MKUU WA WILAYA YA MBOGWE MKOANI GEITA.

DC Mbogwe Mkoani Geita Mariam Seif
Na:Shaban Njia
Mkuu wa Wilayani Mbogwe Mkoani Geita Mariam Seifu amesema kuwa kuna ongezeko kubwa la wahamiaji haramu ambao ambao wanatoka nchi jirani kinyume cha sheria.

Seifu alibainisha hayo jana wakati akizungumza na wandishi wa Habari ofisini kwake ambapo alibainisha kuwa hali hiyo imekithiri wilayani humo kutokana na ukosefu wa ofisi za uhamiaji jambo ambalo linailazimu Wilaya yake kuazima Maofisa wa idara ya Uhamiaji kutoka Wilaya ya Bukombe.

Kutokana na hali hiyo, Seifu alibainisha kuwa Wilaya ya mbogwe bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya wimbi la wahamiaji haramu kutoka nchi jirani za Rwanda,Burundi na Congo ambao wanaoingia nchini bila kufuata taratibu za Kisheria.

"Kumekuwa na idadi kubwa ya wakimbizi katika Wilaya yetu ambao hukimbilia katika vijiji vya kata ya Lugunga na kutengeneza makazi ya kuishi kinyume cha sheria huku wakijifanya ni raia wa Tanzania". Alisema Seifu.

Hata hivyo alitoa agizo kwa wale wote ambao si raia wa Tanzania ambao wanaishi kinyume cha sheria Wilayani humo, kufika katika ofisi za Uhamiaji katika Wilaya ya Bukombe kwa ajili ya kufuata taratibu za kuishi hapa nchini huku akionya kwamba atakaekiuka agizo hilo sheria itachukua mkondo wake.

Aidha aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na viongozi mbalimbali wa serikali za vitongoji, Vijiji na wilaya pindi wanapomtilia mashaka mtu au watu ambao siyo raia wa Tanzania na kwamba hali hiyo itasaidia kupunguza wimbi la wahamiaji haramu Wilayani humo na nchini kwa ujumla.

No comments:

Powered by Blogger.