WATU WAWILI WAPOTEZA MAISHA MKOANI SHINYANGA KATIKA MATUKIO MAWILI TOFAUTI YA KUSIKITISHA.
(Picha Haihusiana Na Matukio)
Na:Shaban Njia
Watu wawili wamepoteza maisha katika matukio mawili tofauti katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo mmoja ameuwawa na mume wake kutokana ugomvi wa mali huku mwingine akiangukiwa na gogo la mti akiwa na wenzake wakiwa katika hatua ya kulibeba kwa ajili ya kwenda kupasua mbao.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa matukio hayo, katika tukio la kwanza mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Mwajuma Ngata Mkazi wa Kata ya Zongomela aliuwawa na mume wake Ntaki Mheziwa kwa kumpiga na nyundo kichwani na kumsababishia kifo chake papo hapo.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa sita usiku ambapo Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ya Zongomela Ally Matisho alisema kuwa ugomvi wa wanandoa hao ni wa muda mrefu na ulikuwa ukisababishwa na mgawanyo wa mali za familia.
Katika tukio la pili nalo pia lilitokea jana ambapo kijana mmoja ambaye jina lake na mahali anapoishi havikufahamika mapema, alifariki baada ya kuangukiwa na gogo la mti akiwa katika harakati za kulisafirisha kwenda kiwandani kwa ajili ya shughuli za upasuaji wa mbao.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa kijana huyo ambae anasadikiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 24 na 25 alikuwa na wenzake wawili ambao hata hivyo baada ya mwenzao kupondwa na gogo walikimbilia kusijulikana.
Miili ya marehemu wote wawili imechukuliwa na jeshi la Polisi na kupelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya taratibu nyingine wakati jeshi hilo likiendelea na uchunguzi wake juu ya matukio hayo.